Askofu Msonganzila azungumzia maambukizi ya Ukimwi, matumizi ya kondomu

Sunday October 6 2019

Askofu wa jimbo Katoliki la Musoma Michael

Askofu wa jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila akitoa kipaimara kwa waamini wa kanisa Katoliki Mugumu,jumla ya waamini 192 wamepata Sakramenti hiyo. Picha na Anthony Mayunga. 

By Anthony Mayunga, Mwananchi [email protected]

Serengeti. Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma, Michael Msonganzila  amesema matumizi ya kondumu hayawezi kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), kuwataka wananchi kumrudia Mungu.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Oktoba 6, 2019 wakati akitoa sakramenti ya kipaimara kwa waamini  192 wa parokia ya Mugumu Serengeti.

Amesema tathmini itatakiwa kufanyika kubaini sababu za ongezeko la maambukizi hayo kwa maelezo kuwa kampeni za mabilioni ya fedha zinafanyika lakini maambukizi bado yapo.

"Watu wamepumbazwa na matumizi ya kondomu kama kinga kumbe inawachochea kufanya zinaa zaidi na matokeo yake maambukizi yanazidi na waathirika wakubwa ni wanawake" amesema.

Askofu amesema matumizi ya kondomu hayakubaliwi na kanisa hilo,  kwamba halipingani na Serikali na Serikali kuhusu matumizi yake, “Bali (kanisa) linaangalia kwa undani athari za kuwaaminisha watu kuwa ni kinga.”

Amesema wasichana wenye umri mdogo baadhi wamekuwa na matatizo kwa kuingia katika ndoa wakiwa wadogo jambo alilodai kuchangia maambukizi.

Advertisement

"Tunatakiwa kumuomba Yesu atuongezee imani  ili kuyashinda majaribu kama haya, maana kinacholeta shida ni tamaa za mwili walio katika ndoa kushindwa kuwa waaminifu," amesema.

Amewataka wazazi kuachana na tabia ya kulazimisha kuwaoza watoto wao kwa ajili ya tamaa za kujipatia mali.

“Ndoa ni tendo la hiari kikanisa na kiserikali, acheni tabia hizo watoto waweze kusoma na kufikia malengo yao,” amesema.

 

Advertisement