Chadema walalamikia mambo tisa uchaguzi, Jafo akemea rafu

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi Serikali ya Mtaa wa Ngoto, Martha Sikalangwe (kushoto) akimkabidhi mgombea uwenyekiti wa serikali ya mitaa huo kwa tiketi ya chama cha ACT-Wazalendo, Hamza Ally fomu ya kugombea nafasi hiyo, katika Manispaa ya Morogoro, jana. Picha na Juma Mtanda

Dar es Salaam. Vyama vya upinzani vimedai kufanyiwa mchezo mchafu katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa, kwamba wagombea wao wanabughudhiwa katika kuchukua fomu, huku Chadema ikitaja maeneo tisa yenye matatizo.

Tayari uongozi wa Chadema umewasilisha barua ya malalamiko tisa kwenda ofisi tofauti ikiwamo ofisi ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kulalamikia ukiukwaji wa kanuni unaodaiwa kufanywa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi katika mitaa na vijiji vilivyopo katika zaidi ya kata 50 ndani ya mikoa 21.

Pia nakala nyingine za barua hiyo iliyosainiwa na kaimu katibu mkuu wa Chadema, Reginald Musini zimewasilishwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ofisi ya Tamisemi na ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni wakishinikiza hatua zichukuliwe ili kuwezesha uchaguzi huo ufanyike kwa huru na haki

“Hali hii ni kinyume cha kanuni na ukiukwaji wa Katiba ya 1977, ambayo malengo yake ni uwepo wa serikali za mitaa, upelekaji wa madaraka kwa wananchi na kuimarisha demokrasia maeneo husika,” inasema barua hiyo.

“Ni rai yangu ofisi yako itachukua hatua ili chama kishiriki uchaguzi huo.”

Hali hiyo inajitokeza katika siku ya pili ya wagombea kuchukua na kurejesha fomu za kugombea nafasi ya uenyekiti wa mtaa, kijiji, kitongoji na nafasi tano za wajumbe wa halmashauri ya kijiji au mtaa.

Fomu hizo zinatolewa na ofisi ya mtendaji wa mtaa ambaye anatambulika kama msimamizi msaidizi wa uchaguzi, hadhi inayoendana na kujaza fomu namba 2, 3 na 4 ya tamko la maadili ili kuwahakikishia wadau kuwa uchaguzi utaendeshwa katika misingi ya haki na usawa.

Hata hivyo, Chadema imedai kuwa wagombea wake wamepewa fomu zisizo na nembo ya halmashauri katika baadhi ya maeneo, kunyimwa fomu za kugombea licha ya kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa, kufungiwa ofisi licha ya muda kuruhusu kikanuni na kupitishwa wagombea feki wa Chadema.

Madai mengine ya Chadema ni wagombea kutochangia michango ya mwenge, ofisi nyingi kutofunguliwa hadi jana mchana, kunyimwa fomu za maadili, kudaiwa kukosa sifa ya ukazi licha ya kuwa na sifa ya kupiga kura na wengine kunyimwa fomu kwa madai ya kujiandikisha mara mbili.

Pia maeneo mengine, Munisi alidai, wagombea wao walitakiwa kuwa na vitabu vya stakabadhi ili kupewa fomu na wengine Sumbawanga mkoani Rukwa walinyimwa fomu kwa madai kuwa hakukuwa na taarifa zao kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi.

Madai hayo yalithibitishwa na Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo aliyesema kuna changamoto zimejitokeza katika hatua ya uchukuaji fomu za wagombea.

Akizungumza jana jijini Dodoma, Jafo alisema kuna dosari zimejitokeza katika baadhi ya maeneo na kuwataka watendaji wajirekebishe.

Jafo alitoa kauli hiyo jioni, ikiwa ni saa chache baada ya Chadema kudai kuwasilisha barua ya kulalamikia ukiukwaji wa kanuni na ukandamizaji kwa baadhi ya wagombea wao.

Katika ufafanuzi wake, Waziri Jafo alisema alipokea malalamiko katika kata 72 kwa nchi nzima na tayari timu ya uchaguzi ya Tamisemi inashughulikia na kuagiza pia kamati za rufaa wilayani kufanya kazi hiyo.

“Ni kweli huko Liwale tumesikia kuna shida, tumetoa maelekezo ya nini kifanyike ili kuondoa hali hiyo. Uchaguzi huu ni wa upendo hivyo tunapaswa kupendana wote,” alisema Jafo.

John Mrema, ambaye ni mkurugenzi wa mawasiliano wa Chadema, alisema jana wafuasi wa chama hicho makao makuu ya wilaya ya Mbozi walianza kuandamana wakidai wasimamizi wa uchaguzi wafungue ofisi ili wagombea wao wachukue fomu badala ya kutumia majina feki.

Moshi na Dodoma

Mjini Moshi, Lain Kamendu, ambaye ni msimamizi wa uchaguzi wa manispaa, Juma Tukosa (Moshi Vijijini) na Erick Kaaya (Mwanga) walidai mwamko ni mkubwa katika uchukuaji fomu huku katibu wa CCM wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya akidai wagombea wao karibu wote wamechukua fomu.

Katibu wa Chadema wa mkoa, Basil Lema alisema wagombea wao wanaendelea kuchukua fomu huku changamoto ndogondogo zilizojitokeza zikishughulikiwa.

Mkoani Dodoma, makamu mwenyekiti wa CUF-Bara, Maftaa Nachumu alidai kuwepo ukiukwaji wa kanuni katika maeneo mengi nchini, kama wapinzani kunyimwa fomu za kugombea huku wa CCM wakipewa kupitia mabalozi.

Balozi ni ngazi ya kwanza ya uongozi iliyozoeleka katika mfumo wa CCM, akitakiwa kusimamia nyumba kumi.

Maftaa alisema siku nzima ya jana katika wilaya ya Liwale watendaji wa vijiji waliamua kufunga ofisi zao na kuondoka ili wapinzani wasiweze kuchukua fomu.

CCM watifuana

Kwingineko, kutokana na maagizo ya kurudia mchujo wa kupata wagombea katika baadhi ya maeneo ndani ya CCM, wagombea 25 wa nafasi za ujumbe katika kijiji cha Kahunda na wagombea sita wa uenyekiti katika vitongoji sita kati ya wanane waligoma kuchukua fomu jana.

Wagombea hao wanailalamikia halmashauri kuu ya wilaya ya Sengerema kurejesha jina la mgombea waliyedai hakuwa na baraka za wananchi.

Hata hivyo, jana kamati kuu ya wilaya ya chama hicho ilitoa taarifa ikisema ikithibitisha kuwa taratibu zilivunjwa kwa hila, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa katiba na kanuni zinazoongoza masuala ya uchaguzi, maadili ya viongozi na utumishi katika chama.

“Chama kimeridhishwa na mchakato wa chama wa kuwapata wagombea wa CCM katika uchaguzi huo. Maeneo ambayo taratibu za uchaguzi hazikufuatwa, taratibu za kikatiba na za kikanuni ziendelee ili kuhakikisha haki inatendeka kama ilivyo asili na desturi ya chama,” inasema taarifa hiyo iliyosainiwa na katibu wa itikadi, siasa na uenezi ya CCM, Humphrey Polepole.

Waitara: Muda bado upo

Naye naibu waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara alijibu hoja hizo akisema baadhi ya watendaji lazima waendelee kushiriki katika majukumu mengine ya kutatua kero za wananchi.

“Kwa hiyo muda bado upo wa kujaza fomu hizo. Leo (jana) ni siku ya pili hadi tarehe 4,” alisema.

Kuhusu wagombea ambao hawatambuliwi na vyama hivyo lakini wamechukua fomu, Waitara alisema inakuwa vigumu kutambua ukweli ni upi kuhusu madai hayo. “Kama mgombea amejitambulisha kutoka chama hicho wakati amekuja na fomu hana kitambulisho cha chama unajuaje ni feki? Pengine kuna mgombea ameshinda hawajamteua kwa hiyo hatuwezi kuingilia mambo ya ndani,” alisema Waitara.

Waitara, aliyeahidi kufanyia kazi baadhi ya malalamiko hayo, pia aliwataka wagombea kufuatilia kwa ukaribu viongozi waliopo ngazi ya wilaya badala ya kuanza kulalamika mitandaoni.

“Siwezi kutatua tatizo lililopo kwenye kijiji. Inabidi nifuatilie lakini pia haisaidii kulalamika mitandaoni,” alisema.