Jafo: Vyama ndio vimejitoa uchaguzi Serikali za mitaa sio wagombea

Muktasari:

Waziri wa Tamisemi nchini Tanzania, Seleman Jafo amesema vyama vya siasa ndio vimejitoa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa sio wagombea.

Dodoma. Waziri wa Tamisemi nchini Tanzania, Seleman Jafo amesema vyama vya siasa ndio vimejitoa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa sio wagombea.

Amesema wagombea wote waliokata rufaa na kushinda, wakiwemo wa vyama vilivyojitoa, majina yao yatapitishwa kugombea katika uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 24, 2019.

“Katika uchaguzi wa mwaka 2019 wagombea waliojitokeza na kuchukua fomu ni 550,036 na ambao walirejesha fomu kwa wakati ni 539,953 sawa na asilimia 97.29.”

“Kwa hiyo ambao hawakurejesha fomu labda kwa sababu mbalimbali au kwa matakwa yao binafsi ni 10,083 sawa na asilimia 2.1 tu” amesema Jafo  leo Jumamosi Novemba 9, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Chadema na ACT-Wazalendo vimejitoa katika uchaguzi huo kwa maelezo kuwa mchakato wake umegubikwa na mizengwe ikiwa ni pamoja na wagombea wao kuenguliwa na ukiukwaji wa kanuni na taratibu.

Katika maelezo yake ya leo,  Jafo amesema ni demokrasia kwa  vyama kujitoa kwenye uchaguzi huo, “ni uhuru wao wala hawalazimishwi kufanya kitu ambacho hawako tayari kukifanya.”

Amesema leo ndio siku ya mwisho kwa kamati za rufaa kupitia rufaa za wagombea wote waliopeleka malalamiko yao, kwamba zinasimamiwa na makatibu tawala wa Wilaya. Amesema zaidi ya rufaa 13,500 zimepokelewa nchi nzima.

“Kwa hiyo kesho tutapata idadi kamili ya wagombea ambao wamepitishwa kugombea  nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi huo kwani hata wale waliokata rufaa na kushinda watatangazwa hiyo kesho,” amesema Jafo.

Amesema hata wagombea wa vyama vya siasa waliojitoa kwenye uchaguzi huo kama walikata rufaa na wakashinda rufaa hizo watatangazwa na majina yao yataandikwa kwenye karatasi za kupigia kura.