Meya wa Chadema Jiji la Arusha atimkia CCM, Lema asema alihama tangu 2016

Muktasari:

Meya wa Chadema Jiji la Arusha, Calist Lazaro amekihama chama hicho na kujiunga na CCM leo Jumanne Novemba 19, 2019.

Dar es Salaam. Meya wa Chadema Jiji la Arusha, Calist Lazaro amekihama chama hicho na kujiunga na CCM leo Jumanne Novemba 19, 2019.

Kwa uamuzi wake huo, Lazaro amepoteza udiwani, umeya, uenyekiti wa mameya na madiwani wote wa Chadema na ujumbe wa kamati kuu ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

Lazaro ametangaza uamuzi wake huo leo katika ofisi ndogo za makao makuu ya CCM Lumumba jijini Dar es Salaam, kueleza kuwa amechukua uamuzi huo baada ya kupitia wakati mgumu akiwa meya wa Jiji hilo.

Taarifa iliyotolewa na katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole inaeleza kuwa Lazaro amehama Chadema kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupokea barua za onyo za Chadema akitakiwa kutoshirikiana na viongozi wa Serikali.

“Mambo hayo ndio yamesababisha kujivua nafasi zake zote  Chadema na kujiunga na CCM. Pia amechukizwa na chama chake kujitoa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa unaowanyima fursa mamilioni ya wapenda demokrasia haki ya kushiriki katika uchaguzi, “inaeleza taarifa hiyo.

Inaeleza kuwa Lazaro yupo tayari kupokea maelekezo ya kazi kutoka kwa viongozi wa CCM.

Akizungumzia uamuzi wa Lazaro, mbunge wa Arusha Mjini (Chadema),  Godbless Lema amesema alijiunga na CCM miaka mitatu iliyopita.

“Mwenendo, moyo na tabia zake zote zilikuwa CCM lakini mwili ndio umewasili leo. Jana usiku nilipokwenda kumpokea mkewe wangu Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) nilikutana na Lazaro akaniambia anakwenda Australia, lakini moyoni nilijua anakwenda Dar es Salaam kwa kazi hii ya leo,” amesema Lema.

Kwa mujibu wa Lema, kuna diwani mmoja ambaye ni rafiki wa karibu wa Lazaro anaweza kujiunga CCM na kwamba kinachombakisha Chadema kwa sasa ni ukaribu wake na mwanachama mtiifu wa chama hicho.