Atupwa jela maisha kwa kunajisi mtoto mwenye ulemavu

Muktasari:

Mshtakiwa alipofikishwa mahakamani alikiri kosa na kuiomba Mahakama itoe adhabu kulingana na sheria kwa iliyopo.

 


Serengeti. Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Serengeti imemhukumu kifungo cha maisha Machabo Mokoro (19) mkazi wa Parknyigoti kwa kosa la kumnajisi mtoto wa kike wa miaka tisa mwenye ulemavu wa akili.

Hakimu mkazi, Adelina Mzalifu ametoa adhabu hiyo leo Alhamisi Novemba 21 baada ya mshtakiwa kukubali kosa.

Mzalifu amesema kosa hilo ni kinyume cha kifungu 130(1)(2)(e) na 131(1) cha kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Awali, mwendesha mashtaka wa Serikali, Renatus Zakeo alisema mshtakiwa alitenda kosa hilo Novemba 20, 2019 saa nane mchana nyumbani kwa mtoto huyo.

Amesema baada ya kumaliza kutenda unyama huo alitoweka.

Hata hivyo, alikamatwa kwa ushirikiano wa wananchi.

Amesema baada ya kufikishwa polisi alikiri na baada ya kufikishwa mahakamani na kukiri kosa, ameomba Mahakama itoe adhabu kulingana na hitaji la sheria kwa kosa aliloshtakiwa nalo.