Rais Magufuli apokewa kwa shangwe uwanja wa CCM Kirumba

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amewasili ni mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika maadhimisho yanayofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mwanza. Rais wa Tanzania, John Magufuli ameingia Uwanjani wa CCM Kirumba Mwanza jijini Mwanza huku akipokewa kwa shangwe na vigeregere kutoka kila kona ya uwanja huo uliofurika.
Rais Magufuli ameingia uwanjani hapo saa 3: 14 asubuhi leo Jumatatu Desemba 9, 2019 akiwa kwenye gari la wazi akiongozwa na pikipiki nane gari moja mbele na nyingine nyuma.
Ameingilia mkono wa kushoto mwa uwanja na kuuzunguka akiwapungia wananchi mikono huku akishangiliwa kila alipopita wakati ukiimbwa wimbo wa taifa.
Baada ya kushuka katika gari la wazi, Rais Magufuli alipanda jukwaa maalum lililokuwa limeandaliwa kisha ukapigwa wimbo wa Taifa ulioambana na mizinga 21. Hata hivyo, ulipopigwa mzinga wa kwanza watu walisikika wakipiga kelele kwa kushangilia wengine wakionekana wakishangaa wakitaka kuangalia mizinga hiyo inapotokea.
Hata hivyo, kadri ilivyoendelea kupigwa mizinga hiyo wananchi walionekana kuzoea tofauti na ilivyokuwa kwa mizinga mitatu ya awali.
Wimbo wa Taifa ulipomaliza kupigwa, Rais Magufuli amekagua gwaride hilo lenye vikosi vya ulinzi na usalama.
Viongozi mbalimbali wamewasili akiwamo; Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassa, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi na marais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi.
Wengine ni mawaziri wakuu wastaafu wa Tanzania, Frederick Sumaye, John Malecela, Mizengo Pinda, Edward Lowassa, Spika wa Bunge mstaafu, Anne Makinda na Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai.
Pia, kuna mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania pamoja na wakuu wa mashirika ya kimataifa.
Viongozi wa kisiasa waliopo ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa DP, John Cheyo, Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally.
Rais Magufuli alipopanda jukwaani, amesalimiana na viongozi hao wote na wengine waliojitokeza.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi