LIVE: Vita ya Daudi na Goliath Chadema

Muktasari:

Freeeman Mbowe hajawahi kuwa na hali ngumu katika uchaguzi wa mwenyekiti wa Chadema tangu aanze kugombea nafasi hiyo.

Na hata leo, Cecil Mwambe hatarajiwi kumpa upinzani mkubwa mwenyekiti huyo anayewania kipiundi cha nne kuongoza Chadema, chama kikuu cha upinzani.


Dar es Salaam. Freeeman Mbowe hajawahi kuwa na hali ngumu katika uchaguzi wa mwenyekiti wa Chadema tangu aanze kugombea nafasi hiyo.

Na hata leo, Cecil Mwambe hatarajiwi kumpa upinzani mkubwa mwenyekiti huyo anayewania kipiundi cha nne kuongoza Chadema, chama kikuu cha upinzani.

Chochote kitakachotokea tofauti na uzoefu huo itakuwa ni muujiza? Litakuwa jambo litakalosumbua vichwa vya wanasiasa wengi na baadhi ya wanachama ambao wanataka aendelee na wadhifa huo.

Mbowe na Mwambe leo watapigiwa kura wakati wa mkutano mkuu utakaofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam ukiwahusisha wajumbe na wageni waalikwa zaidi ya 1,300.

Vita ya wawili ni sawa na pambano maarufu la kwenye kitabu cha Biblia baina ya kijana mdogo aliyeitwa Daudi na mbabe aliyekuwa na mwili wa mkiraba minne aliyeitwa Goliath.

Daudi alitumia silaha ndogo aina ya kombea kumshinda Goliath, jambo ambalo halitarajiwi kutokea kwa Mbowe, mwanasiasa mzoefu aliyeijenga Chadema kufikia hatua ya kuwa chama kikuu cha upinzani, mbele ya Mwambe, ambaye ndio kwanz ana miaka minne tangu ajiunge na chama hicho.

Wawili hao wana historia tofauti.

Wakati Mbowe anayekiongoza chama hicho kutoka mwaka 2004 atawaomba wajumbe wa mkutano huo wamuongezee miaka mingine mitano, Mwambe atakuwa na kazi ya kuwashawi wapiga kura kuwa chama kinahitaji mtu mpya.

Duru za kisiasa bado zinampa nafasi kubwa Mbowe kutetea nafasi hiyo kutokana na hali ya kisiasa aliyopitia tangu achukue chama hicho, na hasa katika siasa za sasa ambazo wapinzani wanaona zinahitaji mtu jasiri, msukumo uliowafanmya vijana wa chama hicho kujitolea Sh1 milioni za kulipia fomu na kumchukulia fomu ili agombee tena.

Na akionekana kutegemea nguvu hiyo, Mbowe alisema jana wakati wa kufungua mkutano wa Baraza Kuu katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, kuwa hataki “kupiga kampeni, lakini Chadema wataamua hatma ya chama chao si mtu aje atupangie kitu”.

“Wanachama na viongozi kazi yetu ni kujenga chama si kujijenga sisi. Nawapongeza hasa kwa mazingira tuliyonayo lakini tuko imara, yaani leo ni bora kuliko kesho,” alisema mbunge huyo wa Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

“Kiongozi yeyote wa chama au nje ya chama atakayechafua umoja wetu hatutamvumilia. Wenzetu wa CCM wanaijadili Chadema zaidi badala ya chama chao.”

Mbowe anayeomba kupewa miaka mitano mingine, alishika nafasi hiyo mwaka 2004 akiwa mwenyekiti wa tatu tangu chama hicho kianzishwe baada ya Edwin Mtei aliyefuatiwa na Bob Makani aliyemuachia nafasi mbunge huyo wa Hai.

Mbowe aligombea urais mwaka 2010 na kushika nafasi ya tatu nyuma ya Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Jakaya Kikwete aliyetetea kiti hicho alichotwaa mwaka 2005.