Polisi wamsaka mwimba injili akidaiwa kumuua mkewe kwa shoka

Muktasari:

Moses Pallangyo anatafutwa na jeshi la polisi mkoani Arusha akidaiwa kumuua mke wake kwa kumkata shoka leo Jumatano Desemba 25,2019.

Arusha. Jeshi la Polisi  Mkoa wa Arusha  nchini Tanzania linamtafuta Moses Pallangyo akidaiwa kumuua kwa kumkata shoka mkewe Marry Richard Mushi mkazi wa kijiji cha Kilinga wilayani Arumeru mkoani humo.

Kamanda wa polisi mkoa Arusha, Jonathan Shana amesema tukio hilo limetokea leo Jumatano Desemba 25, 2019 mchana kutokana na ugomvi wa kifamilia.

"Baada ya kufanya mauaji ametoroka na tunamsaka lakini chanzo kamili cha ugomvi hakijulikani lakini  taarifa za awali zinaeleza huenda ni wivu wa mapenzi," amesema Shana

Pallangyo ambaye ni maarufu kwa jina la Moses Lebaba ni mwimbaji wa kwa za Kiinjili mkoani Arusha.

 Baba wa mtuhumiwa, Latiaeli Pallangyo anasema tukio hili limetoka ikiwa ni wiki tatu tangu marehemu aanze kuishi na mwanae kama mke na mume.

"Hapakuwapo na ugomvi wowote na walitegemea kusherehekea sikukuu ya Krisimasi vizuri.  Mara baada ya Marry kupika chai aliendelea na shughuli za kawaida mpaka mauti yalipomfika kwa kupigwa na shoka chumbani kwake," amesema

Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Jerry Muro  alifika katika eneo la tukio mbali na kutoa pole kwa wananchi wa kijiji cha kilinga,  amesema tayari vyombo ya usalama vimeanza msako mkali wa kumtafuta mtuhumiwa .

Murro amewataka  wananchi kuwa watulivu na kuviachia vyombo vya usalama kufanya kazi yake na kuwataka wananchi wenye kujua taarifa za alipokimbilia mtuhumiwa wasaidiane na vyombo vya usalama.