Washtukia mtandao wa kuuza watoto

Thursday December 26 2019
mtandao pic

Yerevan, Armenia . Kiongozi anayelenga kufanya mageuzi makubwa nchini Armenia ameagiza kufanya uchunguzi mkubwa dhidi ya mradi wa kuuza watoto unaosadikiwa kuwepo kwa muda mrefu, ukihusisha vigogo wa hoispitali na wizara ya afya.
Wakati akisema hayo, msichana mwenye umri wa miaka 35, Syuzan Patvakanyan amekuwa akimsaka binti yake tangu madaktari walipomlazimisha aachane naye takriban miongo miwili iliyopita.
Msichana huyo ametoa simulizi yake kwa AFP baada ya mamlaka nchini Armenia kumkamata daktari maarufu wa magonjwa ya wanawake na ambaye pia ni mkunga, kiongozi wa kituo cha watoto yatima na maofisa wengine, ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa mradi wa biashara ya kisiri ya kuuza watoto ambayo inaaminika kuwa imekuwa ikiendeshwa kwa miaka kadhaa.
Kiongozi mwanamageuzi wa Armenia, Nikol Pashinyan ameagiza uchunguzi wa kina dhidi ya mradi huo ambao alisema anaamini umekuwa ukifanya kazi kwa miaka mingi.
"Inawezekanaje mradi kama huu kuwepo Armenia?" alihoji Pashinyan katika mkiutano wa serikali mwezi huu.
Katika ripoti ya mwaka 2017, shirika la Human Rights Watch lilisema maelfu ya watoto wa nchini Armenia walitenganishwa na wazazi wao bila ya sababu za maana na kuwekwa vituoni.
Zaidi ya asilimia 90 ya watoto walio katika vituo wana angalau mzazi mmoja anayeishi, lilisema.
Kwa mujibu wa wizara ya kazi ya Armenia, kwa sasa chini ya watoto 650 wanaishi katika vituo vya yatima. Zaidi ya asilimia 70 ya watoto hao wana ulemavu, kwa mujibu wa Unicef.
Katika mkasa wa msichana huyo aliyelazimishwa kumsalimisha binti yake kichanga, daktari huyo bingwa anayeitwa  Razmik Abramyan, ametuhumiwa kuhusika akiwa pamoja na wengine kuwa walimshinikiza Patvakanyan amucha binti yake baada ya kumzaa.
Alikuwa na umri chini ya miaka 20 wakati alipoingia kwenye mapenzi na mwanamume ambaye alikuwa anamzidi umri kwa miaka mitano, alisema.
Baada ya kujifungua mtoto wa kike wakati huo akiwa na umri wa miaka 16, madaktari walitishia kumshtaki baba wa mtoto huyo polisi kwa kuzaa na msichana mdogo na wakamshinikiza Patvakanyan kusaini nyaraka za kuonyesha anaridhia kumkabidhi binti yake huyo anayeitwa Stella.
"Nililia, sikutaka kufanya kitu hicho," alisema Patvakanyan katika mahojiano huku machozi yakichuruzika kutoka usoni kwake.
Alisaini karatasi hizo kwa shinikizo lakini siku tatu baadaye akarejea kwa lengo la kumchukua binti yake kichanga, Stella ili ampeleke nyumbani.
Lakini mtoto huyo kichanga hakuwepo tena hapo. Madaktari wakadai kuwa amepelekwa kituo cha watoto yatimakilichokjo katika mji mkubwa wa pili nchini Armenia wa Gyumri. Lakini, hata huko, mama huyo hakumkuta binti yake.
"Tulibaini kuwa mtoto wetu aliyekuwa amefunikwa aliuzwa kutokea hapohapo hospitalini," alisema mwanamke huyo.
Patvakanyan anaonekana kuwa mmoja wa wanawake wengi wanaonaswa na mtandao wa kuuza watoto wachanga, suala ambalo limesababisha kuanzishwa kwa uchunguzi rasmi katika nchi hiyo masikini iliyokuwa sehemu ya dola ya Urusi.
Mwezi Desemba, wachunguzi walisema wamemkamata Abramyan, sambamba na kiongozi wa wodi ya wazazi katika mji mkuu wa  Yerevan.
Daktari mkuu wa magonjwa ya jinsia aliachiwa siku kadhaa baadaye na kusababisha umma ulalamike.
Kwa mujibu wa mwanasheria, Abramyan anakanusha tuhuma hizo akisema ni za kutunga na kwamba hakujihusisha na biashara hiyo.
Mwanasheria huyo, Samvel Dilbandyan, alithibitisha kuwa Abramyan alisaidia kumzalisha Patvakanyan wakati akijifungua Stella, lakini asingeweza kukumbuka kila kitu kinachotokea wakati akizalisha.
"Ni miaka 20 sasa, anawezaje kukumbuka?" Dilbandyan aliiambia AFP.

Advertisement