Kafulila atoa sababu kuwaondoa waratibu elimu 16 na walimu wakuu 20, awaonya Ma DED

Muktasari:

Katibu Tawala Mkoa wa Songwe (RAS) nchini Tanzania, David Kafulila amesema hawatawavumilia wale wote wanaopaswa kusimamia sekta ya elimu na kuufanya mkoa huo kushuka katika ufaulu na hatua za kinidhamu zitaendelea kuchukuliwa.

Mbozi. Katibu Tawala Mkoa wa Songwe (RAS) nchini Tanzania, David Kafulila amesema sababu zilizomfanya kuwaondoa madarakani waratibu elimu kata 16 na walimu wakuu 20 ni kushindwa kuzifanyia kazi taarifa za ukaguzi hivyo kusababisha kushuka kwa ufaulu wa darasa la saba.

Akizungumza leo Jumatano Januari 1, 2020 na waandishi wa habari ofisini kwake, Kafulila amesema hatua alizochukua ni kuwawajibisha watumishi hao kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya walio chini yao.

Alisema ripoti ya ukaguzi ya mdhibiti ubora wa shule ilibaini upungufu uliyoonekana kwenye ukaguzi hali iliyosababisha kuleta madhara kwa kushuka kwa ufaulu na kusababisha mkoa kushika nafasi ya 21 toka nafasi ya 17 mwaka 2018.

"Nikiwa mtendaji mkuu wa mkoa huu, nimechukua hatua ya kutengua uteuzi wa waratibu elimu kata 16 na kuwaagiza ma DED (wakurugenzi wa halmashauri) kuwashusha walimu wakuu 20 na wengine walimu 48 kuonywa na waratibu elimu kata 60 kuonywa," amesema Kafulila.

Amesema msingi wa uamuzi huo unatokana na kuwa baada ya kupata matokeo mabaya ya darasa la saba aliamua kuitisha ukaguzi maalumu kwa shule 114 ambazo zilifanya vibaya ambapo ukaguzi huo ulibaini kukithiri kwa utoro kwa baadhi ya walimu, makosa ambayo yamejirudia mara kadhaa katika ripoti za ukaguzi wa mdhibiti ubora.

Amesema licha ya kuwashusha madaraka waratibu elimu kata kwa kushindwa atachukua hatua kwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri zote mkoani humo kutokana na kutofanyia kazi maelekezo ya upungufu ambayo hutolewa na wadhibiti ubora wa elimu kila wanapokamilisha ukaguzi wao.

Aidha Kafulila amesema sambamba na hatua hizo pia amewachukulia hatua za kinidhamu watendaji wa kata na vijiji ambavyo shule zao zimefanya vibaya.