Kauli ya Magufuli yawaibua Mbowe, Mbatia na wasomi kuhusu uchaguzi mkuu

Dar es Salaam. Baadhi ya wadau wa siasa wamemuomba Rais John Magufuli kuruhusu mabadiliko ya Katiba ili uchaguzi mkuu uwe wa amani, huru na haki kama alivyowaahidi mabalozi juzi.

Juzi katika hafla ya kukaribisha mwaka, Rais Magufuli aliwaeleza mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa kuwa Serikali imejipanga kuendesha uchaguzi huo kwa amani na kwamba utakjuwa huru na wa haki, huku akiwakaribisha waangalizi wa nje kuja kuufuatilia.

Alitoa kauli hiyo miezi michache baada ya CCM kupata ushindi wa zaidi ya asilimia 90 katika uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa ambao ulisusiwa na takriban vyama nane vilivyodai wagombea wake walikuwa wakifanyiwa mchezo mchafu na wasimamizin wasaidizi.

Pia mara kadhaa vyama vya upinzani vilijitoa katika uchaguzi mdogo wa wabunge na madiwani kutokana na wagombea kukamatwa. kubughudhiwa aumawakala kuzuiwa vituoni, huku katika sehemu kadhaa wagombea wa chama tawala wakitangazwa kupita bila ya kupingwa.

Mmoja wa wanasiasa walioombwa kutoa maoni yao jana kuhusu ahadi hiyo ya Rais ni katibu wa siasa na uhusiano wa kimataifa wa CCM, Kanali Ngemela Lubinga aliyesema kwa kuwa Rais Magufuli amewahakikishia mabalozi kuwa uchaguzi utakuwa huru na wa haki, hakuna haja ya kuwa na wasiwasi.

“Mkuu wa nchi hawezi kutukatisha tamaa,” alisema Lubinga.

“Hakuna haja ya kuwa na wasiwasi. Wenye wasiwasi wa kauli hiyo wanapaswa kuelewa kuwa atakabiliana na changamoto zitakazojitokeza kuelekea uchaguzi mkuu.

Lakini mazingira ya uchaguzi wa serikali za mitaa na chaguzi ndogo yamewafanya wachambuzi na wanasiasa wengine waliofuatwa na Mwananchi kuonyesha wasiwasi na wengi wakitaka mazingira ya uchaguzi yaboreshwe kwa kwanza kuandika katiba mpya.

“Ni sehemu ya propaganda wanazofanya wanasiasa hata wapinzani,” alisema profesa wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bakari Mohamed.

“Mazingira ya sasa hayaruhusu kuwa na uchaguzi huru, labda yabadilike. Ni kitu ambacho hakiwezekani, labda kuwe na mabadiliko katika Katiba, mfumo wa sheria na katika mfumo wa tabia ya vyombo vya ulinzi na usalama, mabadiliko makubwa ya Tume ya Uchaguzi.”

Mhadhiri huyo alitoa mfano wa uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24 mwaka jana akisema ni ushahidi tosha kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 hautakuwa huru wala wa haki.

Alisema njia peke ya kufanya mabadiliko hayo ni wananchi na wadau wote kuweka shinikizo kwa Serikali ili watawala wayakubali.

Maoni kama hayo alikuwa nayo mwenyekiti wa zamani wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, ambaye alisema ahadi hiyo ya Rais ilikuwa ni siasa na kuna wasiwasi kwamba uchaguyzi utakuwa huru na wa haki kama alivyoahidi.

Alisema Rais Magufuli ametoa kauli hiyo wakati madai ya Katiba yaliyoanza tangu mwaka 1992 hayajafanyiwa kazi.

“Kwa hali hiyo unategemea kutakuwa na uchaguzi huru na haki? Kwa sababu aliyemtangulia (Rais mstaafu Jakaya Kikwete) alianzisha mchakato wa Katiba, huyu wa sasa ameusimamisha,” alisema.

“Mimi niseme kwamba hiyo ilikuwa ni siasa na bahati mbaya sisi Waafrika tunachukulia siasa kama kusema mambo ambayo hayawezekani, tukasema yanawezekana.”

Mchakato wa kuandika Katiba mpya, ambao pia ulisusiwa na wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka vyama vya upinzani na baadhi ya taasisi za kijamii, ulikwama katika hatua ya kura ya maoni, na Rais Magufuli alishasema kuwa suala hilo si kipaumbele chake.

“Juhudi zinazofanyika kwa sasa ni kuelekea gizani kabisa,” alisema Kibamba.

“Kuna mifano mingi inayoonyesha kwa sababu tumeua michakato yote ya uwazi kwa mfano Open Governance Partnership (OGP), tumeua (Mpango wa Afrika wa kutathjmini kiutawala bora) APRM, kulikuwa na African Charter on ACDEG, Mkataba wa Afrika wa Demokrasia, Uchaguzi na Utawala Bora).

“Sasa kama mkataba wa Afrika wa Mambo ya uchaguzi Demokrasia na Utawala nchi imegomea kuutekeleza, halafu kiongozi aibuke aseme uchaguzi uwe huru na wa haki? Tutaupima kwa vigezo gani?”

Mbowe: Tunaandaa waraka

Lakini mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliona kuna haja ya kutafakari ahadi hiyo huku akitaka ufafanuzi zaidi.

“Kuna mambo kadhaa ya kutafakari kuhusu kauli hiyo, lakini kama Taifa tunahitaji ufafanuzi wa kauli hiyo kwa kuwa hivi karibuni tu kulikuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa na kile kilichotokea mnajua, lakini Rais akasema ulikuwa uchaguzi wa huru na haki na chama chake kikapongeza,” alisema.

Mbowe alisema kunahitajika mazungumzo ya pamoja ili kuweka mazingira sawa kwa vyama vyote kwa kuwa uchaguzi ni mchakato, akitoa mfano wa Zanzibar ambako alidai wananchi wananyimwa vitambulisho vya ukaazi na hivyo hawataweza kushiriki uchaguzi.

“Wabunge na madiwani wanazuiwa kufanya mikutano kwenye maeneo yao, mimi nimezuiwa, Zitto (Kabwe) amezuiwa, sasa kama vyama vinazuiwa unasemaje uchaguzi utakuwa huru na haki,” alisema.

“Tulitarajia Rais angeita wadau mbalimbali wanaohusika na uchaguzi kuzungumza ili kujiandaa na uchaguzi na hapo ndipo tutaingia kwenye uchaguzi na ukawa huru na haki, lakini si sasa.”

Mbowe pia alizungumzia hatua ambazo chama chake kinachukua kujaribu kurekebisha hali hiyo.

“Chadema tunakusudia kumuandikia barua Rais mambo tunayokusudia yafanyike ili uchaguzi uwe huru na haki. Sasa maridhiano ya wadau wote. Muda si mrefu waraka huo kutoka Chadema kwenda kwa Rais Magufuli watauona”.

Mbatia ampongeza

Lakini mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia alimpongeza Rais Magufuli na kumtaka akubali kukutana na vyama vya upinzani kujadili hali ya siasa.

“Ni kauli nzuri na ya kuleta matumini. Ni kauli ya kujenga umoja wa kitaifa. Kwa kuwa ametamka neno haki kuwe na uchaguzi huru na wa haki, ukipata haki unapata mshikamano,” alisema Mbatia.

Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) amemwomba Raiskutekeleza ndoto hiyo.

“Ili kuwe na taasisi imara, twende kwenye matendo, tuwe na mazungumzo ya pamoja. Japo anasema kuwe na uchaguzi huru na wa haki lakini tunaona yaliyotokea,” alisema mbunge huyo wa Vunjo.

Naye mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, John Shibuda anakusudia kuitisha mkutano kujadili masuala ya uchaguzi.

“Kuna vikao nimeshaitisha vitakavyojadili duru za siasa na uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Kikao hicho kitatoa msimamo wa vyama kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka huu,” alisema.

Naye mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe alitaka mamlaka ya kikatiba ya wananchi ya kuchagua viongozi wao yaheshimiwe.

“Katiba pia inasema mamlaka ya kuchagua viongozi ni ya wananchi, lakini kwa sasa hayo mamlaka hayapo,” alisema.