Corona kusitisha mikutano ya SADC Tanzania

Muktasari:

Kikao cha dharura cha Mawaziri wa Sekta ya Afya katika Nchi za Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika(Sadc) kimelishauri Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo kusitisha ushiriki wa mikutano yote ya kukutana ana kwa ana ikiwa ni tahadhari ya kusambaa kwa virusi vya Corona (COVID-19) na badala yake kuanza kutumia mifumo inayohusisha teknolojia ya mawasiliano

Dar es Salaam. Kikao cha dharura cha Mawaziri wa Sekta ya Afya katika Nchi za Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika(Sadc) kimelishauri Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo kusitisha ushiriki wa mikutano yote ya kukutana ana kwa ana ikiwa ni tahadhari ya kusambaa kwa virusi vya Corona (COVID-19).

Badala yake, kikao hicho chini ya mwenyekiti wake, Ummy Mwalimu ambaye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kimeshauri mikutano itakayoendelea kuanzia sasa ianze kufanyika kwa njia ya mifumo ya kiteknolojia ikiwamo mitandao.

Kikao hicho kimekutanisha mawaziri na watalaamu wa sekta ya afya   kutoka nchi 10 zikiwamo Zambia, Zimbambwe, Afrika Kusini, Malawi, Angola, Namibia, Lesotho chini ya mwenyeji Tanzania kwa lengo la kujadili ajenda ya hali ya mlipuko wa virusi vya corona vilivyofika katika nchi 101 hadi sasa.

“Tumepitisha azimio la kutoa ushauri kwa baraza hilo la mawaziri kusitisha mikutano ya face to face(ana kwa ana) inabidhi tuisitishe kwa muda hadi pale hali itakapokuwa imetulia, badala yake tumeshauri zitumike njia nyingine kama video conference,” amesema Waziri Ummy.

Itakumbukwa, mkutano wa 39 wa jumuiya hiyo uliofanyika Agosti 17 na 18 mwaka jana jijini Dar es salaam ulikabidhi majukumu ya uongozi wa jumuiya hiyo kwa Rais John Magufuli baada ya Rais wa Namibia, Hage Geingob kumaliza muda wake.

Katika tukio hilo, Tanzania ilianza kuratibu na kusimamia vikao mbalimbali vya kamati za watalaamu.

Kwa mujibu wa Sekretarieti ya Jumuiya hiyo, Tanzania ilitarajiwa kuendesha mikutano mbalimbali zaidi ya 400 inayohusisha maamuzi kupitia mijadala mbalimbali ya watendaji, watalaamu, mawaziri wa kisekta na baraza hilo la mawaziri. 

Waziri Ummy amesema  kikao kimejiridhisha nchi moja tu katika Sadc ambayo ni Afrika Kusini ndiyo imeshapata wagonjwa saba hadi kufikia leo jioni. China ambako virusi hivyo vimeanzia kusambaa kwa sasa ina wagonjwa 28 huku kukiwa na wagonjwa 3,633 nje ya China.


Hatua zinazofuata

Wakizungumza kwa vipindi tofauti wakati wa uwasilishaji wa maazimio ya kikao hicho, Waziri Ummy amesema kikao kimeazimia kila nchi mwanachama wa SADC kuanza kujitathmini na hali ya mlipuko wa virusi hivyo, kuanzisha mfumo wa upimaji kwa nchi husika na kushirikiana na mashirika ya kimataifa.

Azimio lingine ni kuanza utekelezaji wa kukabiliana na kusambaa kwa virusi hivyo na si kuchukua tahadhari kama ilivyokuwa awali, kuanzisha ushirikiano na wizara nyingine nne ambazo ni wizara ya utalii, fedha, uhamiaji na wizara ya ulinzi na usalama kwa kila nchi mwanachama ili kudhibiti tishio.

Waziri wa Afya nchini Zimbambwe, Obadia Moyo amesema hatua zinazohitajika kwa sasa katika maandalizi ya kukabiliana na kusambaa kwa ugonjwa huo ni kuanzisha program za mafunzo mbalimbali ya kuelimisha wananchi namna ya kujikinga, kuandaa vifaa maeneo ya vituo vya afya.

Mkurugenzi wa huduma za Afya nchini Afrika Kusini, Dk Moeketsi Modisenyane amesema baada ya kuingia kwa virusi hivyo tayari serikali imeshajipanga kuhakikisha wanadhibiti kusambaa kwa virusi hivyo.

“Kwa wanaoingia wageni tunawafanyia vipimo na tukibaini ana dalili tunamtenga kwa ajili ya uchunguzi zaidi, hadi kufikia leo jioni tayari nimepokea taarifa ya wagonjwa saba wenye maambukizi ya virusi vya corona,”amesema Modisenyane.

Waziri wa Afya wa Zambia, Chitalu Chilufya amesema tayari Serikali ya China imethibitisha kwamba raia wanafunzi wote wanaotoka nchi za Sadc, wako mahali salama nchini China na uangalizi ni wa hali ya juu.

“China inafanya kazi kwa ukaribu sana na Sadc, tunaishukuru sana kwa ulinzi huo, tunawahakikishia raia wote wa Sadc watakuwa salama kabisa,”amesema Waziri Chilufya.

Waziri Chilufya pia amesisita kuhakikisha ushirikiano unaimarishwa katika upatikanaji wa taarifa pamoja na kuimarisha ukaguzi wa hali ya juu katika mipaka ya nchi za Jumuiya hiyo.