Kupika hesabu kwafuata kampuni tano za uhasibu

Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Ludovick Utouh

Muktasari:

Chama cha wahasibu nchini (TAA) kimeeleza kuwa Zaidi ya kampuni tano za uhasibu zilifutiwa leseni mwaka jana huku wahasibu Zaidi ya 12 wakipewa adhabu mbalimbali.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa chama cha wahasibu nchini Tanzania, (TAA) Peter Mwambuja amesema mwaka jana kampuni za uhasibu zaidi ya tano zilifutiwa leseni kwa kosa la kupika hesabu.

Pamoja na kampuni hizo, Mwambuja amesema wahasibu 12 walipewa adhabu mbalimbali kwa makossa akama hayo ambayo yanahusisha uandaaji wa taarifa za fedha zisizo halisi.

Mwambuja amesema hayo leo Machi 11 wakati wa mkutano wa ushauri ulioandaliwa na TAA kwa asili kuwakutanisha wahasibu wakongwe na wanaochipukia ikiwa ni sehemu ya sherehe za wiki ya wahasibu nchini ambayo ilianza Machi 9.

“Jukumu la kwanza la TAA ni ulezi ndiyo maana leo tumewakutanisha wakongwe na wanaochipukia pamoja na hivyo tunalo jukumu la kuhakikisha wahasibu hawatoki katika misingi na mwaka jana tuliwashughulikia kadhaa,” amesema.

Amesema miongoni mwa walioshughulikiwa mwaka jana walikuwa wamelalamikiwa na benki pamoja na Mamlaka ya mapato nchini (TRA). “Wahasibu nafasi (rank) ya juu tuliwashusha chini waanze upya”.

Katika mkutano huo umehudhuriwa na mwanachama wa TAA na Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Ludovick Utouh ambaye amesema ni muhimu endapo kuna mwanachama wa TAA anayeenda kinyume na miiko ya uhasibu atolewe taarifa ili aadhibiwe.

Kuhusu maendeleo ya sekta uhasibu amesema hivi sasa kunahitaji wahasibu wengi wenye weledi na waadilifu kwani kadri uchumi unavyokuwa ndivyo watu wa kada hiyo wanavyohitajika.

“Sisi ni tofauti na Madaktari ambao wao wanahitajika kulingana na wingi wa watu sisi mahitaji yetu yanatokana na ukuaji wa uchumi,” amesema.

Mwenyekiti wa bodi ya wahasibu na wakaguzi wa hesabu nchini (NBAA) amesema mhasibu anapaswa kuwa mtu mwadilifu ambaye anaongeza thamani kwa jamii inayomzunguka.

“Tukifanya kazi zetu vizuri tutawavutia vijana wengi Zaidi kuingia katika fani hii, kazi yetu sio kuzia fedha wala kuwa ‘back ofice’,” amesema.

Mkurugenzi Mkazi wa kampuni ya uhasibu ya EY, Joseph Sheffu amesema wafanyabiashara wengi hususani wadogo hawajui faida ya kutunza kumbukumbu sahihi za fedha na katika wiki hii ya uhasibu elimu inaendelea kutolewa ili wafahamu kwa manufaa ya biashara zao na uchumi wa nchi.