Lipumba aahidi tekonolojia ya uvuvi Mtera

Muktasari:

Mgombea huyo alisema samaki wana soko kubwa duniani na nchini na mahitaji yao ni makubwa, vijana wakiwezeshwa kuwafuga kwa wingi kwa teknolojia ya kisasa, tatizo la ajira litapungua kwa kiwango kikubwa katika maeneo yenye mito mikubwa na mabwawa.

Isimani. Mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema akichaguliwa, atapenyeza teknolojia mpya ya ufugaji na uvuaji samaki katika Bwawa la Mtera lililopo mkoani Iringa.

Teknolojia hiyo amesema itasaidia kupunguza ukosefu wa ajira hasa kwa vijana nchini. Sambamba na hilo, ameahidi kutoa mtaji wa ufugaji samaki ili kuongeza uzalishaji na tija.

Aliyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Migoli, Jimbo la Isimani alikokuwa akiomba kura jana.

“Najua hapa Iringa kuna wavuvi wa samaki katika Bwawa la Mtera lakini wengi wao wameshindwa kuendelea na shughuli za uvuvi kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya kukamatwa na ushuru mkubwa. Tunahitaji kulinda mazingira yenu ili haki ziweze kutendeka, tupeni kura zenu wavuvi muweze kupumua na kuwapunguzia ushuru na shughuli zenu ziweze kuendelea katika hali nzuri,” alisema Profesa Lipumba.

“Najua vijana wengi hamna ajira, niwahakikishie wavuvi wote hapa Mtera, ipo teknolojia nzuri ya kufuga samaki hasa kwenye mabwawa makubwa kama hili la Mtera, tunaomba kura zenu ili tuweze kuwapenyezea teknolojia hiyo mpya ya ufugaji samaki, tuwape mtaji wa kufuga samaki muweze kuongeza uzalishaji na mpate kipato kizuri cha kukidhi mahitaji yenu,” alisema.

Mgombea huyo alisema samaki wana soko kubwa duniani na nchini na mahitaji yao ni makubwa, vijana wakiwezeshwa kuwafuga kwa wingi kwa teknolojia ya kisasa, tatizo la ajira litapungua kwa kiwango kikubwa katika maeneo yenye mito mikubwa na mabwawa.

“Tupeni kura zenu tukayasimamie mambo haya tuwape vijana wetu uwezo wa kutumia teknolojia bora kuzalisha samaki kwa wingi. Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya ajira kwa vijana na hii ni moja ya suluhisho,” alisema Profesa Lipumba.

Gazeti hili lilizungumza na baadhi ya vijana waliohudhuria mkutano huo ambao walieleza changamoto wanazokabiliana nazo ukiwamo ukosefu wa ajira.

“Vijana wengi hapa hatuna ajira, maisha yetu magumu sana na wapo wengine waliomaliza mpaka vyuo vikuu tunao hapa lakini hawana ajira. Ahadi kama hizi kama kweli zikitekelezwa, basi itakuwa mkombozi kwetu,” alisema Mussa Rajabu mkazi wa Migoli.

Alisema ahadi za mgombea wa CUF zinafariji na kuonyesha mwanga kwa sababu vijana wengi wa eneo hilo ni wavuvi, wakiwezeshwa kuwa na mabwawa ya kufugia yatawainua kiuchumi hivyo kuondokana na utegemezi kwa ndugu au marafiki hivyo kushiriki katika maendeleo ya Taifa lao.

Naye mgombea ubunge wa chama hicho Isimani, Nasma Upetu aliwaomba wananchi wa jimbo hilo kumchagua ili akawasilishe kero zao na kusimamia utatuzi wake kwa manufaa ya wananchi wote.

“Najua mkutano wa leo sio wangu lakini wananchi wa Isimani msifanye makosa, nichagueni mimi Oktoba 28 nikawasilishe kero zenu. Nitumeni nikawatumikie na mpigieni kura nyingi Profesa Lipumba kwa sababu ana ndoto kubwa ya kuwatumikia kwa dhati,” alisema Nasma.