Dk Mwinyi aahidi kuipandisha hadhi Hospitali ya Micheweni kuwa ya wilaya

Muktasari:

Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk Hussein Mwinyi amesema ili wananchi washiriki kikamilifu shughuli za ujenzi wa nchi, ni lazima wawe na afya bora na vyanzo vya mapato vya uhakika

Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk Hussein Mwinyi amesema ataipandisha hadhi Hopitali ya Michweni  kuwa ya wilaya pamoja  na kuwaajiri madaktari bingwa ili wananchi wapate huduma bora za afya.
Ahadi hiyo ameitoa katika mwendelezo wa mikutano ya kampeni aliofanyika katika uwanja wa mikutano wa Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema ataimarisha sekta ya afya kwa kuongeza ununuzi wa dawa na kuajiri wataalamu mbalimbali wa sekta ya afya.  
Amesema ili wananchi washiriki kikamilifu shughuli za ujenzi wa nchi, ni lazima wawe na afya bora na vyanzo vya mapato vya uhakika.
Kuhusu kilimo, Dk  Mwinyi amewaahidi wakulima wa karafuu na mwani kuwa endapo atachaguliwa kuwa Rais, atajenga viwanda vikubwa kwa ajili ya kuchakata mazao  hayo ili kuyaongezea  thamani na kuwanufaisha wakulima hao.
Kwa upande wa sekta ya elimu, ameahidi kuajiri walimu wa masomo ya sayansi na hesabu  na kujenga shule za kisasa ili kuongeza ufaulu.
Dk Mwinyi kuwapatia kazi mbadala vijana wanaochonga matofali na kusababisha uharibifu wa mazingira kwa kuwapatia mitaji na mikopo ili wafanye shughuli nyingine.
Makamu mwenyekiti wa CCM, Dk Ali Mohamed Shein amewataka wananchi wa kisiwani Pemba kuwapigia kura wagombea wa chama hicho ili waendeleze mambo mema yaliyoasisiwa na Serikali ya awamu ya saba.
 “Dk Mwinyi ni mtu makini asiyependa kukurupuka au kusema sema ovyo kama walivyo baadhi ya wagombea wa vyama vingine vya kisiasa,"alisema Dk ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdulla Juma amesema chama hicho kimeendelea kufanya kampeni za kistaarabu kwa kueleza namna kitakavyotekeleza sera zake kwa vitendo.