VIDEO: Simulizi baba aliyepoteza mke, watoto watatu na mdogo wake

VIDEO: Simulizi baba aliyepoteza mke, watoto watatu na mdogo wake

Muktasari:

Siku ya tukio, mtoto huyo aliyesalia, Erick anayesoma shule ya Green Hill iliyoko Pugu, alikuwa amepelekwa shuleni kuanza kulala bwenini, takribani saa nne kabla ya moto kushika nyumba yao iliyopo mtaa wa Pugu Stesheni, ikawa ndiyo nusura yake.

Dar es Salaam. Uchungu uliopitiliza. Ndivyo picha unayoipata kutoka katika simulizi ya Edward Katemi, baba aliyepoteza watoto watatu, mke na mdogo wake katika ajali ya moto iliyotokea jijini Dar es Salaam Oktoba 13.

“Sasa nimebaki na mtoto mmoja anayesoma darasa la sita,” alisema Katemi katika mahojiano maalum na Mwananchi.

Siku ya tukio, mtoto huyo aliyesalia, Erick anayesoma shule ya Green Hill iliyoko Pugu, alikuwa amepelekwa shuleni kuanza kulala bwenini, takribani saa nne kabla ya moto kushika nyumba yao iliyopo mtaa wa Pugu Stesheni, ikawa ndiyo nusura yake.

“Nilisikia watoto wangu watatu, mke wangu na mdogo wangu wakilia kuomba msaada. Ni uchungu usioelezeka,” alisema Katemi ambaye alieleza kuwa vifo hivyo vilitokana na marehemu kukosa hewa.

“Nilipambana kuhakikisha naokoa familia yangu pamoja na msaada wa majirani, lakini ilishindikana.”

Waliofariki katika moto huo ni Jackline Frank, ambaye ni mkewe, Esther mwenye miaka 15 (mdogo wake na mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Pugu) pamoja na watoto wake watatu; Edwin (mwanafunzi wa Shule ya Msingi Pugu Station, Edison (Green Hill) na Ivon mwenye umri wa miaka minne.

Katemi, ambaye ni mfanyabiashara, alisema pamoja na nyumba kuteketea, anaamini vifo hivyo vilitokana na moshi uliotanda ndani. Alisema siku ya tukio hilo, alikuwa ndio anawasili nyumbani kwake Pugu saa 3:58 usiku akitokea kazini kwake.

“Umeme haukuwepo. Nilipofika nyumbani na nilipotaka kupiga honi nifunguliwe geti, umeme ulirudi ghafla kisha ukakatika,” alisema Katemi.

“Nilipoteremka kwenye gari ukarudi lakini ndani kwangu tu haukuwaka. Ghafla niliona cheche zikitoka sebuleni eneo ilipo main switch na ghafla moshi mkubwa ukaanza,” alisema.

Katemi alisema kwanza hakusikia chochote lakini baada ya sekunde chache alisikia mkewe na watoto wakiomba msaada na sebuleni moto ulishatanda.

“Kila kitu kilishashika moto, hivyo walishindwa kutoka. Nilisaidiana na majirani kuzima moto na maji na baada ya kufanikiwa kuuzima ilibidi kutoboa chumba cha watoto na nilifanikiwa kuwatoa wawili na baadaye mdogo wangu Esther, moshi mzito ulitanda ndani. Tulimwaga maji zaidi kumfikia mke wangu chumba kingine na mtoto mdogo wa kiume.”

Katemi alisema walipowatoa wote hawakuwa na majeraha ya moto na walikuwa wakipumua kwa mbali.