Wasanii zaidi 200 kushiriki tamasha Dodoma

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa atakuwa mgeni rasmi katika tamasha la Karibu Dodoma Festival litakalofanyika Oktoba 24 mwaka 2020 katika Uwanja wa Jamhuri

Dodoma. Zaidi ya wasanii 200 nchini watashiriki tamasha la Karibu Dodoma Festival linalotarajia kufanyika Oktoba 24, 2020.

Mratibu wa tamasha hilo, Simon Mwapagata amesema leo Jumatano Oktoba 21 2020 kuwa tamasha hilo litafanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini na mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Amesema lengo la tamasha hilo ni kumpongeza Rais John Magufuli na Serikali anayoingoza kwa kazi alizozifanya katika kipindi cha miaka mitano na kutambulisha miradi ya kimkakati iliyofanywa na Serikali.

“Lengo lingine ni kuhamasisha shughuli za kiuchumi na uwekezaji katika mkoa wa Dodoma,”amesema Mwapagata.

Amesema shughuli nyingine za tamasha hilo zitakuwa ni pamoja na kufanya matembezi ya amani kwa lengo la kuhamasisha amani wakati wa uchaguzi.

Mwapagata amesema pia, watatoa zawadi ya heshima kwa Rais Magufuli kwa kazi aliyoifanya na mchezo wa mpira wa miguu wa kirafiki kwa watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu.

Amesema tamasha hilo litajumuisha burudani kwa siku nzima na wasanii wa muziki kutoka Dodoma watahusika, vikundi vya ngoma za kitamaduni vya mikoa ya jirani, wasanii wa bongo movie.

Amewataja baadhi ya wasanii ni Bambo, Mtanga, Masantula, Kiwewe, Mama Kanumba  na Full tanki.

Wasanii wa bongo flavor watakaohudhuria ni wasanii wa singeli, hip pop, taarabu, rusha roho na gospel.

Tamasha hilo limeandaliwa na Taasisi ya The Ambassador for the Development Intiative (AFDI), Taasisi ya Karibu Dodoma Festival, Jasiri Asili pamoja na Jumuiya ya Watu wenye Ulemavu.