Mwalimu: Tutatoa kipaumbele kwa watu si wanyamapori

Mwalimu: Tutatoa kipaumbele kwa watu si wanyamapori

Muktasari:

Mgombea mwenza wa Chadema, Salum Mwalimu amesema chama hicho kikiibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020 kitatoa kipaumbele kwa watu si wanyamapori ikiwa wanyama hao watavamia makazi ya wananchi na kufanya uharibifu.

Meatu. Mgombea mwenza wa Chadema, Salum Mwalimu amesema chama hicho kikiibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020 kitatoa kipaumbele kwa watu si wanyamapori ikiwa wanyama hao watavamia makazi ya wananchi na kufanya uharibifu.

Mwalimu amesema Serikali ya chama hicho itachukua jukumu la kuwalipa fidia wananchi hao.

Mwalimu amesema hayo leo Ijumaa Oktoba 23, 2020 wakati wa mkutano wake wa kampeni katika kata ya Tindabuligi jimbo la Kisesa, ambako aliwataka wananchi kukichagua chama hicho.

"Tutasogeza hili pori la akiba (Maswa) ili mpate malisho ya mifugo yenu na ikitokea tembo akaingia katika makazi ya wananchi akaharibu mali au mazao, Serikali ya Lissu (Tundu-mgombea urais wa Chadema) itatoa fidia," amesema Mwalimu.

Amesema Serikali ya Lissu itatenga maeneo ya kutosha kwa ajili ya malisho ya mifugo na haitakamata  ng'ombe wala mbuzi wa mwananchi eti kisa wamelishwa kwenye porini lililotengwa.

"Leo hii haiwezekani tembo akivamia mali zetu na kuziharibu Serikali ionekane iko sawa lakini mwananchi kumdhibiti tembo huyo iwe kosa la ujangiri. Hatuwezi kuthamini tembo kuliko uhai wa wananchi wetu," amesema Mwalimu.

Mgombea ubunge wa Chadema, Kisesa Kishabi amesema Serikali iliyopo sasa haijawatendea haki wafugaji, wakulima wa pamba ndiyo maana bei ya pamba imeshuka na wafugaji wamehamisha mifugo yao hivyo wananchi wanahitaji mabadiliko.