Mtihani wa ACT kukubali maridhiano Zanzibar

Muktasari:

Tafsiri kupitia tamko la Rais mteule wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, baada ya kutangazwa mshindi, inaweza kujenga taswira kuwa kiongozi huyo anaweza kuwa na dhamira ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Dar es Salaam. Tafsiri kupitia tamko la Rais mteule wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, baada ya kutangazwa mshindi, inaweza kujenga taswira kuwa kiongozi huyo anaweza kuwa na dhamira ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Hata hivyo, mtihani upo kwa mpinzani wake, Maalim Seif Sharif Hamad na chama chake cha ACT-Wazalendo kutoa uamuzi ndani ya siku saba baada ya Rais kuapishwa.

Akizungumza baada ya kutangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji mstaafu Hamid Mahmoud Hamid kuwa Rais mteule wa Zanzibar, Dk Mwinyi alisema ataendeleza maridhiano yaliyopo kikatiba.

Alisema atadumisha amani iliyopo kwa kushirikiana na wapinzani kwa sababu wao ni nyenzo muhimu katika kukuza demokrasia nchini.

“Nipo tayari kuyaendeleza maridhiano yaliyopo katika katiba yetu, kwani Zanzibar ni kubwa na muhimu kuliko tofauti zetu, nitashirikiana nanyi kujenga Zanzibar mpya,” alisema Dk Mwinyi.

Akiwa ameshinda kwa zaidi ya asilimia 76.2 alisema kuwa amepokea ushindi kwa mikono miwili na akaahidi kuijenga Zanzibar kwa ushirikiano na Wazanzibari wote bila kujali itikadi.

Hata hivyo, kwa mwongozo wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010, ACT-Wazalendo wanapaswa kuketi na Dk Mwinyi ndani ya siku saba kisha kumpa jina la mtu wanayempendekeza kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, vilevile kufanya mashauriano kuhusu muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kauli hiyo ya Dk Mwinyi, pamoja na ile nyingine kwamba “Zanzibar ni kubwa na muhimu kuliko tofauti za kisiasa”, inaweza kujenga picha ya utayari wake wa kushirikiana na wapinzani wake kuunda Serikali.

Mtihani ni Seif ambaye awali alitangaza hatamtambua aliyetangazwa kama Rais wa Zanzibar, vilevile uchaguzi uliompa ushindi.

Seif alisema uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 27 na 28, haukuwa uchaguzi, bali zoezi la kijeshi. “Uchaguzi ulitekwa na vyombo vya dola. Ikiwa kulikuwa hakuna uchaguzi vipi nitamkubali aliyetangazwa? Hakuwekwa madarakani na wananchi kama Katiba inavyotaka. Amewekwa madarakani isivyo halali,”alisema.

Pamoja na msimamo wake huo, bado Seif jana alipozungumza na Mwananchi kwa simu kuhusiana na msimamo wake juu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, alirejesha mpira kwa chama chake kwamba ndicho kitakachokuwa na uamuzi wa mwisho.

“Kwanza itategemea huyo aliyetangazwa! Akiamua kuunda GNU na kutaka kutushirikisha sisi itategemea maamuzi ya Chama. Si maamuzi yangu,” alisema.

Kauli hiyo ya Seif, imeshabihiana na ile ya Mkuu wa Itikadi na Uenezi wa ACT-Wazalendo, Salim Bimani aliyesema: “Chama kitakaa na kutoa tamko la pamoja kuhusu vurugu zote hizi za uchaguzi. Kwa sasa hatuwezi kuzungumzia ushiriki wetu kwenye hiyo Serikali ya Umoja wa Kitaifa.”

Mtihani ulipo

Kwa mujibu wa Ibara ya 39 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010, uteuzi wa Makamu wa Kwanza wa Rais kutoka chama kilichoshika nafasi ya pili kwenye uchaguzi wa Rais, si hiari kwa Rais aliyeshinda, bali ni lazima pale mshindi wa pili anapopata kura za urais asilimia 10 au zaidi.

Katika matokeo ya urais Zanzibar yaliyotangazwa Oktoba 29, mwaka huu na Jaji Hamid, Seif aliyegombea urais kupitia ACT-Wazalendo, amepata asilimia 19.87, ambayo ni karibu mara mbili ya asilimia zinazohitajika ili chama kilichoshika nafasi ya pili kitoe Makamu wa Kwanza wa Rais na kushiriki kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Ibara hiyo inaeleza bila kutaja idadi, kuwa endapo mshindi wa kiti cha urais hakuwa na mpinzani, basi Makamu wa Kwanza wa Rais atapatikana kupitia chama kitakachoshika nafasi ya pili kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Hadi sasa, kabla ya kupitisha majina ya viti maalumu, CCM ina viti 49 na ACT-Wazalendo kimoja.

Kwa ufafanuzi huo wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010, mantiki yake ni kuwa ACT-Wazalendo ndiyo wenye kutakiwa kutoa majibu ya mtihani wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ama wakubali au wakatae.

Na kwa mujibu wa Katibu, wanapaswa kuwa na majibu ndani ya siku saba kutoka siku ambayo Dk Mwinyi ataapishwa.

Kingine kinachoweza kuwapa mtihani ACT-Wazalendo kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni idadi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Mpaka sasa wana mjumbe mmoja ambaye ndiye pekee ana sifa ya kuteuliwa kabla ya kungoja viti maalum au hisani ya uteuzi katika viti 10 vya Rais wa Zanzibar.