Magufuli awatuliza wabunge nafasi za uwaziri

Rais John Magufuli

Muktasari:

Amesema hakuna haraka ya kuteua mawaziri kwa kuwa wengi wana sifa

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema bunge la sasa lina wabunge wengi wa chama chake, hivyo hakutaka kufanya uteuzi wa haraka huku akiwataka wabunge kushusha ‘presha’.

“Kwa sababu kazi tuliyoomba ni ubunge wala siyo uwaziri, tulitoka hapa tulienda kuomba ubunge kuwa tutawatumikia wananchi wetu na kukabidhiwa ilani sasa mengine yanatoka wapi?”

Amesema nafasi za mawaziri na manaibu waziri haziwezi kufika 30 hivyo katika watu 350 (wabunge) hata angekuwa mtu mwingine angepata shida kubwa kufanya uteuzi.

“Kazi ni ngumu ni lazima utende haki na lazima umtangulize Mungu kuwa anayestahili usije ukamuonea, hivyo nawaomba mnisamehe kuwa nachukua muda mrefu,”

Amesema mwaka 2015 kazi ilikuwa rahisi kwa sababu wabunge wa CCM walikuwa wachache hivyo uwanja wa yeye kuchagua ulikuwa ni mdogo.

“Hawa wawili si kwamba wao ni maarufu sana kuliko waliobaki (Dk Philip Mpango na Profesa Palamagamba Kabudi), mwaka 2015 hawakuwa na majimbo na niliwaambia waende katika majimbo au walikotoka wakaenda,”

Kuhusu kumteua Dk Mpango kuwa Waziri wa Fedha kwa haraka, amesema hiyo ni kwa sababu fedha zitahitajika na haziwezi kusubiri miezi mitatu au minne ndiyo maana akaona anafaa akamrudisha kutokana na mafanikio yaliyofanyika katika uongozi wake.