22 jela miezi sita kwa uzururaji, kujihusisha na biashara ya ngono

Muktasari:

  • Mahakama ya Mwanzo Nunge manispaa ya Morogoro imewahukumu watu 22 kifungo cha miezi sita jela baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la uzembe na uzururaji.

Morogoro. Mahakama ya Mwanzo Nunge manispaa ya Morogoro imewahukumu watu 22 kifungo cha miezi sita jela baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la uzembe na uzururaji.

Baada ya hakimu Emelia Mwambagi kusoma hukumu hiyo, washtakiwa hao ambao wengi ni wanawake waliangua kilio mahakamani, kuomba kusamehewa.

Kesi hiyo ilisikilizwa jana Jumatano Agosti 28, 2019 kwa zaidi ya saa tano dhidi ya wasichana wanaodaiwa kufanya biashara ya ngono pamoja na wanaume wanaodaiwa kujihusisha na ushoga.

Washtakiwa hao walikamatwa usiku wa Agosti 16, 2019  eneo la Kahumba manispaa ya Morogoro.

Hakimu Mwambagi aliieleza mahakama hiyo kuwa adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa washtakiwa hao na wengine wanaotumia miili yao kujidhalilisha na kuwadhalilisha wazazi, ndugu na jamaa kwenye maeneo wanayotoka.

Hakimu Mwambagi aliieleza mahakama kuwa washtakiwa wote waliokamatwa ni vijana wenye uwezo wa kufanya kazi za kuwaingizia kipato halali lakini wamekuwa wakizurura na wengine wakitumia vibaya miili yao.

Kabla ya kutoa hukumu hiyo hakimu Mwambagi aliwaachia huru washtakiwa sita kutokana na utetezi wao pia vielelezo walivyoviwasilisha mahakamani hapo kudhihirisha kuwa hawahusiki na shtaka hilo.

Katika utetezi wao washtakiwa hao walidai  walikamatwa kwenye nyumba za kulala wageni walipokwenda kujipumzisha baada ya kutoka safari, huku wengine wakidai kukamatwa katika maeneo yao ya kazi wakidai kuwa wanajihusisha na biashara ya kuuza chakula.