ACT-Wazalendo yaendelea kupata viongozi wapya

Muktasari:

Dorothy Semu na Juma Duni  Haji wamechaguliwa kuwa makamu wenyeviti wa Tanzania Bara na Zanzibar katika mkutano mkuu wa chama hicho ulioingia siku ya pili leo katika ukumbi wa Mlimani City.

Dar es Salaam. Wajumbe wa mkutano mkuu wa ACT-Wazalendo wamewachagua Dorothy Semu  na Juma Duni Haji kuwa makamu wenyeviti wapya wa chama hicho, Tanzania Bara na Zanzibar.
Dorothy kabla ya kuchaguliwa nafasi alikuwa ni kaimu katibu mkuu wa ACT- Wazalendo, wakati Duni  alikuwa naibu kiongozi wa chama akimsaidia Zitto kwenye majukumu hayo.
Wawili hao wamechaguliwa leo Jumapili Machi 15, 2020 kwenye mkutano mkuu huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City wilayani Ubungo jijini hapa.
Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Uchaguzi ya ACT- Wazalendo, Omar Said Shaaban amesema jumla ya wajumbe 372 walishiriki mchakato huo kati ya hao 367 walipiga kura kwa wagombea hao watano waliokuwa wakiwania nafasi hiyo.
"Dorothy amepata kura 267sawa na asilimia  71.38, Mary Mongi kura 13, Juma Mkumbi 23 na Edgar Mkosamali 61 hawa ni upande wa Tanzania Bara. Zanzibar mgombea alikuwa mmoja ambaye ni Duni aliyepigia kura za ndio 354 sawa 98.36," amesema Shaaban.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa mchakato huo, Duni amewashukuru wajumbe wa mkutano huo kwa kuonyesha imani kwake na  kumpigia kura za ndio.
"Nashukuru zaidi wajumbe na Wazanzibari kwa kutonipa mshindani na nimekuwa peke yangu. Nawaahidi wanaACT-Wazalendo sitonunulika kwa sababu mimi sio bidhaa bali binadamu mwenye  anayehitaji kuheshimiwa," amesema Duni.
Dorothy ameungana na Duni akiwashukuru wajumbe wa mkutano kwa kumchagua akisema ameipokea nafasi hiyo kwa unyeyekevu mkubwa akiwahidi kuwatumika kwa utumishi uliotutuka.
Kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo, usiku wa kuamkia leo wajumbe hao walimchagua kwa kishindo Maalim Seif Sharif Hamad kuwa mwenyekiti wa pili wa chama hicho huku Zitto akitetea nafasi yake ya kiongozi wa chama kwa mara nyingine.