Abiria ndege ya Air Tanzania iliyozuiwa kuondoka Afrika Kusini watafutiwa usafiri mwingine

Muktasari:

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL),  Ladislaus Matindi amesema abiria wa ndege ya Air Tanzania iliyozuiwa kuondoka katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo, Johannesburg nchini Afrika Kusini wametafutiwa usafiri mbadala

Dar es Salaam. Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL),  Ladislaus Matindi amesema abiria wa ndege ya Air Tanzania iliyozuiwa kuondoka katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo, Johannesburg nchini Afrika Kusini wametafutiwa usafiri mbadala.

Taarifa ya kuzuiliwa kwa ndege hiyo iliyokuwa ikitoka Afrika Kusini kwenda Dar es Salaam, Tanzania ilitolewa jana Ijumaa Agosti 24, 2019 na katibu mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Leonard Chamuriho.

Alibainisha kuwa inashikiliwa kwa amri ya mahakama kuu ya Gauteng, Johannesburg na Serikali inafuatilia suala hilo ili iweze kuachiwa mara moja.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Agosti 24, 2019 Matindi amesema abiria wote waliokuwa katika ndege hiyo wametafutiwa usafiri mwingine, wapo walioanza kuwasili jijini Dar es Salaam.

“Tutahakikisha abiria wote waliokata tiketi  wanasafiri kama ilivyopangwa, huwa kuna makubaliano katika mashirika ya ndege kwamba unapopata tatizo kama hili nani anakusaidia.”

“Suala la kupeleka ndege nyingine kwa safari ya Afrika kusini itategemea ni jambo la kusubiri suala lenyewe kwanza liwe wazi  kujua kwa nini kimetokea na nini kinafuata. Hili ni suala la kisheria hivyo itatokana na namna litakavyokuwa limetatuliwa lakini sisi tutaendelea kuihudumia hiyo njia.”

Matindi amesema kuna safari zitaathirika kutokana na kushikiliwa kwa ndege hiyo moja aina ya Airbus A220-300 na abiria ambao tayari wamekata tiketi wataarifiwa iwapo katika safari husika kutakuwa na mabadiliko yoyote au ipo kama ilivyopangwa.

Amesema jambo hilo halina uhusiano wowote na kilichotokea siku ya kwanza ya uzinduzi wa safari hiyo, ambapo ilielezwa kuwa ujumbe wa ATCL ulizuiliwa kuingia nchini humo kwa ajili ya hafla ya kuzindua rasmi safari.