Adaiwa kujinyonga kwa hasira baada ya mkewe kuuza kondoo na kumnyima fedha

Geita. Paulo Hassan, mkazi wa kijiji cha Gamash, kata ya Bulela wilayani Geita, anayekadiriwa kuwa na zaidi ya miaka 40 anadaiwa kujinyonga na shuka kwa kile kinachodaiwa kuwa ni hasira baada ya mkewe kuuza kondoo na kutumia fedha bila kumshirikisha.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, mke wa marehemu, Jenipha Lateremla alidai kuwa mumewe alijinyonga usiku wa kuamkia Januari 18 baada ya kutokea ugomvi baina yao.

Jenipha alisema usiku wa Januari 17 wakiwa chumbani, mumewe alianza kuhoji alikopeleka kondoo, alimueleza kuwa alimuuza kwa ajili ya maandalizi ya Sikukuu ya Krismasi na fedha hizo alizitumia kwenye sikukuu.

“Tukiwa tumelala usiku, akaniambia tena, unajua moyo wangu ulivyo na hasira, hela umefanyia nini nilivyoona hivyo kwa kuwa akikasirika huwa ananipiga nilitoka nje nikamuacha,” alisema Jenipha.

Alisema alipotoka nje mumewe alifunga mlango na mkewe akabaki nje na kuwagongea watoto na asubuhi watoto walipoamka walimgongea baba yao kwa ajili ya kumsalimia, lakini hakuitikia na walipochungulia ndani walikuta amejinyonga kwa shuka yake ya kulalia.

Diwani wa Viti Maalum wa Bulela, Salome Kitura (CCM) alisema polisi wametoa kibali cha familia kuutoa mwili na kuuzika.

Kitura aliishauri jamii kujizuia pindi wanapokuwa na hasira na wajenge tabia ya kutafuta ushauri wanapokuwa na jambo linalowasumbua badala ya kujichukulia sheria mkononi.

Jitihada za kumpata kamanda wa polisi mkoani hapa, Mponjoli Mwabulambo kuzungumzia tukio hilo hazikufanikiwa baada ya simu yake ya mkononi kutopokelewa licha ya kupigwa kwa mara tatu tofauti.