Dk Mwigulu: Dunia imebadilika, kutegemea misaada kumepitwa na wakati
Muktasari:
- Dunia ya sasa inahitaji mataifa kujenga uchumi imara unaotegemea rasilimali na mapato ya ndani badala ya kusubiri misaada
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba amesema enzi za kutegemea misaada kugharamia maendeleo na huduma za kijamii zimepitwa na wakati, akisisitiza umuhimu wa Watanzania kujenga utamaduni wa kujitegemea na kuwajibika kutatua changamoto zao wenyewe.
Dk Mwigulu amesema dunia ya sasa inahitaji mataifa kujenga uchumi imara unaotegemea rasilimali na mapato ya ndani badala ya kusubiri misaada.
Amesema hayo kwenye harambee ya ukamilishaji wa jengo la kitega uchumi la Kanisa Anglikana Tanzania iliyofanyika kanisa kuu la Roho Mtakatifu Dayosisi ya Central Tanganyika Dodoma, leo Jumapili Juni 21, 2026.
Akizungumza katika ibada hiyo, amesema ujumbe uliotolewa na askofu wakati wa mahubiri kuhusu mabadiliko ya dunia umeakisi mwelekeo wa Serikali wa kujenga uchumi unaojitegemea.
"Mambo ya misaada yamekwisha kupitwa na wakati. Nadhani nchi yetu ilipata pata misaada ambapo kulikuwa na dawati linalosimamia fedha za misaada, kulikuwa na misaada ikiwamo makapu mbalimbali ya kisekta, hayo sasa kwenye bajeti yetu hayapo tena na Rais anaendelea kusisitiza kuwa na bajeti inayotegemea rasilimali za ndani ya nchi,” amesema.
Amesema jambo hilo lieleweke vizuri linatakiwa iwe ni lugha na wimbo wa kila Mtanzania huku akisema mwelekeo huo unaonekana wazi katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 ya Sh62.3 trilioni ambayo imejikita zaidi kwenye ukusanyaji wa kodi, magawio kutoka taasisi za umma na vyanzo vingine vya ndani.
Akisisitiza zaidi amesema Serikali haitaki kuona huduma muhimu kwa makundi maalumu zikiendelea kutegemea misaada kutoka nje, badala yake jamii na taasisi za ndani zinapaswa kuchukua jukumu hilo.
“Zamani ilizoeleka katika maeneo mbalimbali kuna vituo vya watoto wenye mahitaji maalumu, ilizoeleka kwamba, vituo hivyo vinaendeshwa kwa fedha za misaada kutoka nje na vyenyewe, kwa kuwa eneo hili ni muhimu basi ni vyema sisi serikalini lakini pia na Watanzania wote kuendelea kuachana na dhana hiyo.
“Kwamba watoto wasio na wazazi watatakiwa kutunzwa na wasamaria wema wa mataifa mengine hayo mambo yanaendelea kuisha watoto wa Tanzania wenye uhitaji wanatakiwa watunzwe na Watanzania,” amesisitiza.
Sambamba na hilo, Dk Mwigulu amesema Serikali imeanza kupitia baadhi ya taratibu na kanuni zinazoweza kuzuia utoaji wa misaada ya haraka kwa wahitaji.
Amesema baadhi ya watu wenye ulemavu au wenye uhitaji wanapofika katika ofisi za umma kuomba msaada, wamekuwa wakipewa barua za kwenda kujichangisha badala ya kusaidiwa moja kwa moja.
"Mtu mwenye ulemavu anapoenda katika ofisi ya umma kuomba msaada, hapaswi kutumwa kwenda kuchangisha. Anatakiwa kupata msaada pale pale na kuendelea na maisha yake," amesema.
Kutokana na hali hiyo, amewataka viongozi wa Serikali za mitaa na halmashauri nchini kutambua vituo vya watoto yatima na makundi mengine yenye uhitaji ili viweze kupatiwa msaada kwa urahisi kupitia mifumo rasmi ya serikali.
Hata hivyo, katika mahubiri ya awali mhubiri amesema Tanzania ina kila kitu na ni aibu makanisa ya Tanzania kuandika barua kuomba msaada nje ya nchi.
“Kwa miaka mingi makanisa yameishi kwa kutegemea misaada Ulaya na Marekani,” amesema akiongeza kwamba watu wa huko sikuhizi hawaendi makanisani hivyo ni ngumu kutegemea misaada.
Hivyo amesema kanisa la sasa la Ulaya na Marekani haliwezi kusadia kwakuwa limerudi nyuma.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Maimbo Mndolwa amesema kanisa linakwenda kwa misingi ya enzi ya maandiko matakatifu, mapokeo ya kanisa na matumizi sahihi ya akili.