Dk Mwigulu atangaza kiama kwa wanaonyang’anya ardhi za watu
Muktasari:
- Waziri Mkuu ametangaza kuwashughulikia wale wote wanaokanyaga haki za watu hususan sekta ya ardhi huku akiwataka waliotumia mabavu kunyang’anya warejeshe.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ametangaza kuwashughulikia ‘wanaokanyaga’ haki za watu hususan sekta ya ardhi huku akiwataka wale wote waliotumia mabavu kunyang’anya warejeshe kwa wanaostahili.
Amesema kwenye jamii kuna michezo ya kunyang’anya haki za watu bila kujali huku akiahidi kuwashikisha adabu wote wanaohusika.
Dk Mwigulu amesema hayo leo Jumapili Mei 24, 2026 wakati akisikiliza kero za wananchi wa Wilaya ya Kilolo, Mkoa wa Iringa.
Dk Mwigulu amesema mara kadhaa amekuwa akiwasisitiza viongozi wenzake wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na watumishi wa umma kuhakikisha wanatenga muda wa kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.
Waziri Mkuu aliwahi kuwaagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Waziri wa Tamisemi kukaa kwa dharura na kuja na mapendekezo yatakayomaliza migogoro ya ardhi iliyodumu kwa miaka mingi.
Akiwa Iringa, Dk Mwigulu amesema wanaotumia mabavu kupora ardhi za watu, warejeshe haki kwa wanaostahili na kwamba, anaanza kufuatilia kwa ukaribu mkoa kwa mkoa.
“Wanakwenda kwenye ardhi ya mtu wanachukua eneo lake kujenga shule, kituo cha afya; hawafanyi fidia na siku ya kuzindua shule hata kutambua tu ambaye wamechukua eneo lake hawafanyi hivyo.
“Maeneo mengine wanatumia fedha nyingi za kuzindua, kuzidi hata hela anayodai mwenye shamba. Si mumpe hela yake aendelee na maisha. Watanzania wote wanufaike na matunda ya uhuru wa nchi yao,” amesema.
Amesema wameanza kuwa na watu kwenye jamii wasio na uaminifu; na Serikali inaendelea kuangalia njia bora ya kushughulikia hali hiyo.
“Pia, kuna watu wanaazimishwa mashamba halafu wanayang’ang’ania. Tuanze kufanya utaratibu kwa njia zilizo rasmi, Serikali tunaangalia njia bora ya kushughulikia migogoro ya ardhi inayoanza kutishia undugu wetu,” amesema.
Akisisitiza zaidi, Dk Mwigulu amesema kuna watu wanategemea uadilifu wa viongozi waliopo ofisini, wanaoamua kuhusu maisha yao.
“Ardhi ni urithi, kuna watu wanategemea uadilifu wa viongozi wanaoamua kuhusu maisha yake, ardhi yake, fidia yake na kuamua pale anapoonewa, hii ndio maana ya Serikali,” amesema.
Amesema Tanzania lazima iendelee kudumisha amani kwa kila mmoja ili kutimiza wajibu wake, kuhurumiana na kuzingatia haki.
Mmoja wa wananchi, Merita Joseph akiwasilisha kero kwa Waziri Mkuu amesema amenyang’anywa shamba alilopewa na baba yake mwaka 1970.
“Nilipotaka kuanza kilimo nikaambiwa ni shamba la kampuni. Nilipoanza kufuatilia, nikaitwa hadi shambani lakini hadi sasa sijapata haki,” ameeleza.
Mwananchi mwingine, Beti Agustino amesema eneo la marehemu kaka yake lililojengwa nyumba, limechukuliwa na wanaojiita wawekezaji waliodai kupimiwa na halmashauri.
“Eneo ni la watoto wa marehemu kaka yangu. Nimeshinda kesi ya Mahakama. Mgogoro bado upo, kwa kuwa wamefungua kesi kwa jina lingine na safari hii wameshinda wao kesi,” amesema.
Akijibu sakata hilo, Dk Mwigulu ameagiza kutotolewa kwa hati hadi mamlaka zijiridhishe huku akiagiza kukamatwa kwa hao wanaojifanya wawekezaji.
“Enzi za Nyerere kulikuwa na adhabu za viboko kwa watu wasio na adabu… wengine ni kutandika viboko. Mnasumbua watu,” amesema.
Katika hatua nyingine, kitendo cha mgonjwa kuambiwa akanunue dawa dukani kimemchefua Dk Mwigulu huku akihoji kioski kinatoa wapi dawa ambazo Serikali haiwezi kupata.
Amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha kujenga majengo, kununua dawa na vifaa tiba, pia kuajiri Watanzania ili wawasaidie wenzao lakini kumekuwa na tatizo la dawa.
“Au wameficha dawa za Serikali ili wao wauze? Tutafanya utaratibu wa kuanza kufuatiliana hatua kwa hatua,” amesisitiza.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James amesema mkoa huo una wakulima wengi wanaotegema barabara kuwa kiunganishi kikuu cha kupeleka mazao sokoni ikiwamo mbao.