Adhabu zitakazowakabili Membe, Kinana na Makamba hizi hapa

Muktasari:

Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imeagiza makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, Yusuf Makamba na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje,   Bernard Membe kuhojiwa na kamati ya usalama na maadili ya Taifa kujibu  tuhuma za maadili zinazowakabili kwa mujibu wa katiba ya chama hicho tawala nchini Tanzania

Dar es Salaam. Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imewataka makatibu wakuu wawili wa zamani wa chama hicho na aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje, Bernard Membe kufika mbele ya kamati ya usalama na maadili kujibu tuhuma za maadili zinazowakabili.

Makatibu wakuu hao ni Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba.

Ijumaa iliyopita, Halmashauri Kuu hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli ilikutana jijini Mwanza Desemba 13, 2019 na kutoa maagizo mbalimbali ikiwamo kuwaita viongozi hao.

“Waitwe na Kamati ya usalama na maadili ya taifa ili wajibu tuhuma za kimaadili zinazowakabili kwa mujibu wa katiba ya chama na kanuni ya maadili na uongozi,” ilisema taarifa ya CCM iliyotolea na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole.

Ingawa bado haijafahamika wanachama hao watafika lini mbele ya kamati hiyo yenye wajumbe 12 wakiongozwa na Rais Magufuli, lakini kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la 2017 zimebainishwa adhabu tatu kwa wanachama wanaofika mbele ya kamati hiyo.

Katika kanuni hizo kifungu cha 5 (2) kinasema; wanachama wanaovunja maadili ya chama kama yalivyoainishwa katika katiba ya CCM na kanuni za CCM wanachukuliwa hatua za kuwarekebisha na kama itashindikana kuwarekebisha ni kuwaondoa katika chama au katika uongozi.