VIDEO: Aeleza jinsi Watanzania zaidi ya 400 wanavyoishi mji wa virusi hatari China

Dar es Salaam. Jacob Julius, anayeishi mji wa Wuhan wenye mlipuko wa virusi vya corona, anasema takriban Watanzania 400 wanaishi katika jiji hilo la China na wanachukua hatua kuepuka maambukizi.

Virusi hivyo, vinavyofananishwa na vingine vinavyosababisha ugonjwa wa mapafu (SARS) na ambavyo vilisababisha vifo vya zaidi ya watu 600 mwaka 2002 na 2003, vimeibuka tangu mwishoni mwa Desemba 2019 na husababisha mafua makali huku dalili zikielezwa kuwa ni mwili kupanda joto.

Tayari watu 41 wameshapoteza maisha kutokana na virusi hivyo vipya, huku vifo vitatu vikiripotiwa nje ya Wuhan huku walioambukizwa wakifikia 1,300 na tayari umesambaa katika nchi za Ufaransa, Marekani, Thailand, Japan, Taiwan, Korea Kusini na Macau.

Julius, ambaye ni mwenyekiti wa Watanzania waishio jijini humo, alilieleza Mwananchi jana jinsi wanavyojikinga na maambukizi ya ugonjwa huo kwa kutumia taarifa iliyotolewa na madaktari watatu Watanzania waliopo China.

Wakati Julius akieleza hayo, Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki ameiambia Mwananchi kuwa timu ya wataalam wa afya wa Tanzania waishio nchini humo wanatoa elimu kwa wenzao jinsi ya kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo, vinavyosadikiwa vinatokana na popo, fungo ambaye ni mithili ya paka mwitu na vyakula vinavyotokana na viumbe wa baharini.

Balozi Kairuki alisema wanatambua mchango wa timu hiyo na ubalozi unawasiliana moja kwa moja na Watanzania waliopo katika maeneo yenye changamoto hizo.

“Wameunda timu ya madaktari wa Tanzania wanaoratibu mawasiliano na kutoa elimu kwa jumuiya ya Watanzania waliopo China. Hadi sasa hakuna Mtanzania aliyeathirika,” alisema Balozi Kairuki.

Akizungumzia jinsi wanavyojikinga, Julius alisema kwa sasa wanalazimika kushinda ndani kuepuka kukabiliana na walioambukizwa.

“Njia za kujikinga zimeshauriwa ila wanafunzi wa Tanzania wametakiwa kutozurura hovyo na kupanda usafiri wa umma ambao kwa sasa umezuiwa,” alisema Julius.

“Tunashauriwa kukaa ndani licha ya kuwa sasa ni baridi sana huko nje na pia ni kipindi cha likizo hatuendi darasani.”

Alisema wameshauriwa kuhakikisha maeneo waliyopo yanakuwa safi, kula chakula cha moto, kunywa maji mengi huku wakitakiwa kuepuka kusogeleana na watu ambao hawajui walikotoka.

“Unajua katika mji huu kuna vyuo vingi sana. Nadhani ni mji uliojengwa kwa ajili ya vyuo tu. Hapa kuna Watanzania takribani 400 hivi wanaosomea fani mbalimbali. Kwa pamoja tumeshauriwa kitu kimoja. Hivyo ndivyo ninavyoweza kuwashauri wenzangu,” alisema Julius.

Taarifa ya timu hiyo ya madaktari kwenda kwa Watanzania waishio China imeandaliwa na Dk Khamis Bakari, Dk Hilal Mmed na Dk Jafar Rajab, ambao kwa pamoja wameeleza jinsi ya kujikinga, dalili za ugonjwa huo, walio hatarini kupata maambukizi na chanzo cha ugonjwa.

Dalili za aliye na virusi

Mtu aliyeshambuliwa na virusi vya corona huwa ana homa na mafua makali, kuumwa kichwa, mwili kuchoka, kikohozi, kubanwa mbavu, maumivu ya misuli, vidonda vya koo, kuathirika mapafu, kupumua kwa shida na hata kusababisha kifo.

Ugonjwa huo hauna chanjo wala tiba ya moja kwa moja.

Ili kuepuka maambukizi, watu hushauriwa kufunika mdomo na pua kwa kitambaa safi au nguo wakati wa kukohoa, kugusana na mgonjwa na kuzingatia usafi binafsi. Pia kuwahi vituo vya huduma za afya kama kuna dalili au kutoa taarifa kituo cha huduma endapo ataonekana mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.