Ali Mufuruki atangaza kujiuzulu Uenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Vodacom Tanzania

Muktasari:

  • Mwenyekiti na Ofisa Mtendaji mkuu wa kampuni ya Infotech investment Group, Ali Mufuruki ametangaza kujiuzulu nyadhifa zake za Mkurugenzi huru, Mwenyekiti wa bodi na Kamati ya Uteuzi wa Kampuni ya Vodacom Tanzania kuanzia Desemba 1, 2019.

Dar es Salaam. Baada ya kuhudumu kwa miaka miwili akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, Ali Mufuruki ametangaza kujiuzulu wadhifa huo kuanzia Desemba 1, 2019.

Pia, Mufuruki ambaye ni Mwenyekiti na Ofisa Mtendaji mkuu wa kampuni ya Infotech investment Group ametanagza kujiuzulu nafasi za mkurugenzi huru na kamati ya uteuzi wa kampuni hiyo kuanzia Agosti 1, 2017.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Oktoba 18, 2019 na bodi na kusainiwa na katibu wa kampuni hiyo, Caroline Mduma imeeleza Mufuruki amechukua uamuzi huo ili kupata muda zaidi wa kuendelea na biashara zake.

Taarifa hiyo imesema katika muda wote wa uongozi wake Mufuruki ametoa mchango mkubwa kwa kampuni kwa uongozi wake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo bodi ipo katika mchakato wa kumpata mkurugenzi huru mwingine atakayechukua nafasi hiyo.