VIDEO: Alichokisema Halima Mdee baada ya kutomsalimia Dk Mashinji

Muktasari:

Leo Jumatatu Februari 24, 2020 katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee ni kama alikataa kumsalimia kwa kumpa mkono Dk Vicent Mashinji  aliyekuwa katibu mkuu wa Chadema.

Dar es Salaam. Leo Jumatatu Februari 24, 2020 katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee ni kama alikataa kumsalimia kwa kumpa mkono Dk Vicent Mashinji  aliyekuwa katibu mkuu wa Chadema.

Mdee na Dk Mashinji leo walifika katika mahakama hiyo kusikiliza kesi ya uchochezi inayowakabili pamoja na wenzao saba, akiwemo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika.

Februari 18, 2020 Dk Mashinji alihamia CCM ikiwa ni miezi miwili baada ya Mbowe kutomteua kuwa katibu mkuu wa Chadema na badala yake kumteua Mnyika.

Dk Mashinji aliyevaa shati la drafti na suruali nyeusi, baada ya kufika mahakamani alisalimiana na washtakiwa wenzake kwa kupeana mikono lakini alipofika kwa Mdee ambaye alikuwa akifuatilia jambo katika simu yake ya mkononi hakumpa mkono katibu mkuu huyo wa zamani wa Chadema.

Viongozi nane wa Chadema pamoja na Dk Mashinji wanakabiliwa na mashtaka 13 yakiwamo ya kula njama, kufanya mikusanyiko na maandamano yasiyo halali na ya uchochezi wa uasi.

Alipoulizwa na Mwananchi sababu za kutomsalimia Dk Mashinji, mbunge huyo wa Kawe amesema..., “achana naye ni mnafiki.”

Mbali na Mbowe, Dk Mashinji, Mnyika na Mdee washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni naibu katibu mkuu Salum Mwalimu (Zanzibar); mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa;  mbunge wa Tarime mjini, Esther Matiko; mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.