VIDEO: Alichokisema Mbowe baada ya kuchaguliwa uenyekiti Chadema

Muktasari:

Freeman Mbowe, amewashukuru wajumbe wa mkutano mkuu wa Chadema kwa kumchagua tena kuwa mwenyekiti wa chama hicho, akibainisha kuwa kura alizopata zitakuwa chachu ya kutekeleza malengo yaliyowekwa.

Dar es Salaam. Freeman Mbowe, amewashukuru wajumbe wa mkutano mkuu wa Chadema kwa kumchagua tena kuwa mwenyekiti wa chama hicho, akibainisha kuwa kura alizopata zitakuwa chachu ya kutekeleza malengo yaliyowekwa.

Amesema upinzani ulioibuka katika uchaguzi unatakiwa kuisha baada ya matokeo kutangazwa.

Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Desemba 19, 2019 saa 11 alfajiri baada ya kutangazwa mshindi kwa kupata kura 886 sawa na asilimia 93.5 huku mshindani wake, Cecil Mwambe akipata kura 59 sawa na asilimia 6.2.

Katika uchaguzi huo ulioanza jana Desemba 18, 2019 na kuhitimishwa leo asubuhi ukishuhudia na naibu msajili wa vyama vya siasa, Sisty Nyahoza aliyeondoka ukumbi wa Mlimani City baada ya matokeo kutangazwa, ulikuwa na kila aina ya upinzani licha ya walioshinda kupata kura nyingi.

Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amechaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho kwa kura 930 sawa asilimia 98.8 huku Sophia Mwakagenda ambaye alijitoa wakati akijinadi, akipata  kura 11 sawa asilimia 1.2.

Katika hotuba yake fupi, Mbowe ameshukuru kwa kupatiwa timu nzuri, “uchaguzi ukimalizika tuna wajibu wa kutekeleza majukumu yetu.”

“Kura mlizonipa hazitakuwa na maana kama nikitoka hapa nitaenda kulala au kumpumzika na kusahau uchaguzi. Kura mlizonipa zitaenda kuwa chachu ya kutengeneza malengo ya Chadema.”

“Yapo makosa tuliyoyafanya kwenye utumishi, lakini yasiende kuwa hukumu kwetu bali yawe marekebisho kwenye mienendo yetu. Asante viongozi, timu mbalimbali , poleni kwa kukesha asanteni vyombo vya habari  kwa namna mnavyo habarisha umma kuhusu ndoto za Chadema," amesema Mbowe.

Mbunge huyo wa Hai amewaomba radhi wajumbe wa mkutano huo kwa namna alivyokuwa akizungumza  kwa hisia wakati wa kuomba kura, “pengine nilizungumza kwa hisia isiyostahili. Nikaona sina unyenyekevu mbele, washauri wangu wameniambia  na nakiri sio tabia yangu na naomba radhi wote niliowakwaza. Siyo kawaida yangu  nilihemka kutokana na hali halisi ya mazingira ya siasa ninayoishi, naomba radhi sana wengi sikuwafurahisha.”

“Jambo hili haliondoi ukweli kuhusu unyenyekevu wangu kwenu. Kwa muda mrefu tumejenga Chadema kwa mapenzi makubwa kwa kuheshimiana na kushikamana bila kujali mdogo wala mkubwa.”