Alichokisema Mwinyi kuhusu Magufuli

Rais mstaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi

Muktasari:

Rais mstaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi amewataka wananchi kumchagua mgombea urais kupitia CCM, John Magufuli ili amalize miradi mikubwa ambayo hajaimaliza.

 

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi amewataka wananchi kumchagua mgombea urais kupitia CCM, John Magufuli ili amalize miradi mikubwa ambayo hajaimaliza.

Ameeleza hayo leo Jumanne Oktoba 20, 2020 kwenye mkutano wa kampeni iliyofanyika katika viwanja vya Msikate tamaa vilivyopo kata ya Vingunguti, Dar es Salaam.

Mwinyi ambaye alikuwa rais wa Tanzania mwaka 1985 hadi 1995  amesema Magufuli amefanya mambo makubwa ikiwemo kujenga barabara kwa kiwango cha lami zikiwemo za juu na kuwataka wananchi kumchagua pamoja na wabunge na madiwani wa chama hicho.

“Magufuli amelibadili jiji la Dar es Salaam..., kafanya kazi kubwa sana katupikia wali na kitoweo na hospitali nzuri katufanyia mambo makubwa kwa muda mfupi."

"Serikali mpya ni ya CCM, mambo aliyoyafanya  Magufuli ni mengi na macho yenu yameona na masikio yanasikia kwani ni uongo?  Kwa nini tusimpe miaka mingine mitano ili atuletee  maendeleo," amesema Mwinyi.

Mwinyi amesema alipokuwa rais uchumi ulikuwa chini na kwamaba alifanya machache na kumwachia  hayati  Benjamin Mkapa na baadaye Jakaya Kikwete lakini hawakufika mwisho.

Amesema alipochaguliwa Magufuli amefanya mengi akitolea mfano jinsi Jiji la Dar es Salaam lilivyobadilika.

"Kinachonifurahisha nimeonana na wananchi wa  Ilala ni siku nyingi sana tangu nikiwa kijana hadi sasa nakutana na wengine wamekuwa wazee.”

"Tuendelee kusherehekea mafanikio ya CCM Taifa lipo kwenye harakati za kutafuta uendeshaji wa serikali  mikutano mingi imefanyika ili kuwakumbusha Tanzania tegemeo lao liwe kwa CCM," amesema rais huyo mstaafu.