Alichokisema Rais Magufuli kuhusu Mo Dewji

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amezindua kiwanda cha kusaga nafaka kilicho chini ya kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL), Kusarini jijini Dar es Salaam huku akimpongeza  Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’ kwa kumtaka kuendelea kuchapa kazi kwani Serikali iko nyuma yake.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amemtaka mfanyabiashara maarufu nchini humo, Mohamed Dewji ‘Mo’ kuendelea kufanya uwekezaji na kutangaza namna ambavyo Serikali ya Tanzania inavyowajali na kuwathamini wawekezaji.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Alhamisi Agosti 1, 2019 wakati wa hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kusaga nafaka kilicho chini ya kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL), Kusarini jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo Rais Magufuli amemtaka bilionea huyo kijana namba moja barani Afrika kutorudishwa nyuma na watendaji wanaoweka vikwazo kwa wawekezaji.

“Mo chapa kazi nenda mbele, wala usiwe mnyonge, Tanzania ipo pamoja na wawekezaji. Kazi unayoifanya ni nzuri, uwekezaji uliofanya ni mkubwa, endelea Serikali iko pamoja na wewe.”

“Niwaombe watendaji ndani ya Serikali tusiwavuruge wafanyabiashara wanaotaka kuwekeza nchini,” amesema

Rais Magufuli ametumia fursa hiyo kumuagiza Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa kuwachukulia hatua watendaji wa wizara yake wanaoweka vikwazo kwa wawekezaji.

“Nimepata taarifa kuna baadhi ya wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza nchini wanawekewa vikwazo, wanazungushwa na wengine wanaombwa rushwa.”

“Waziri wa biashara (Bashungwa) kalishughulikie hili kama kuna watendaji wako ndani ya wizara bado hawajaelewa mtazamo wa Serikali wakae pembeni sisi tuendelee,” amesema Rais Magufuli