Alichokisema Simbachawene baada ya kuapishwa

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania,  George Simbachawene ameahidi kushirikiana na viongozi wengine kuleta matokeo chanya yanayotarajiwa na Watanzania na Rais John Magufuli.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania,  George Simbachawene ameahidi kushirikiana na viongozi wengine kuleta matokeo chanya yanayotarajiwa na Watanzania na Rais John Magufuli.

Simbachawene ameapishwa leo Jumatatu Januari 27, 2020 Ikulu, Dar es Salaam baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli kuongoza wizara hiyo. Rais Magufuli pia alimteua mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azzan Zungu

Amechukua nafasi ya Kangi Lugola ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Simbachawene amesema ataviheshimu vyombo vya usalama kufanya kazi yake huku yeye akishughulika na mambo ya utawala.

“Pale ambapo vyombo vinafanya makosa kazi yangu ni kukutaarifu kwamba kuna mambo hayapo sawa, lakini mimi sina cheo chochote na wala sina nyota yoyote na hukunipa nyota hapa lao.”

“Umenipa jukumu nikusaidie katika kusimamia vyombo hivi ambavyo kwa sehemu vinafanya kazi ya ulinzi na usalama na ninatambua mimi sio amiri jeshi mkuu,” amesema Simbachawene ambaye awali alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

Mbunge huyo wa Kibakwe (CCM) amesema Rais Magufuli anatamani kuona vyombo hivyo vinafanya kazi kulingana na wakati wa sasa wa kuelekea katika uchumi wa viwanda.

“Hatuwezi kuwa na vyombo vya ulinzi na usalama vinavyobweteka na kukaa,  lazima vyombo hivi vishiriki katika ujenzi wa uchumi huo kwa kuzalisha na kufanya shughuli zinazoweza kupunguza hata kero zilizopo katika vyombo hivyo,” amesema Simbachawene.

Amebainisha kuwa kuna watu wa kutosha kwenye vyombo hivyo na wakifanya kazi kwa bidii wanaweza kutatua changamoto zilizo kwenye maeneo yao.

“Wanaweza  kujenga nyumba, kuzalisha viwanda katika hilo Rais nitajitahidi kushirikiana na wenzangu,” amesema Simbachawene.

Amesema wizara hiyo ni kubwa ina watendaji wazuri na atashirikiana nao.