Aliyekuwa Makamu wa Rais Zimbambwe akimbilia mafichoni

Muktasari:

Kiongozi huyo ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa Robert Mugabe alitakiwa kujisalimisha katika Tume ya Kupambana na Rushwa kwa ajili ya mahojiano.

Zimbabwe. Makamu wa Rais wa zamani wa Zimbabwe, Phelekezela Mphoko ametoweka baada Tume ya Kupambana na Rushwa ya nchi hiyo (ZACC) kutangaza kumuhoji.

Kiongozi huyo ambaye alitakiwa kujisalimisha katika taasisi hiyo kuhusiana na madai ya rushwa anadaiwa kuondoka wakati gari lake lilipowakaribia maafisa wa taasisi hiyo.

Kiongozi huyo alikuwa Makamu wa Rais chini ya Robert Mugabe kabla ya Serikali kung’olewa madarakani na jeshi la nchi hiyo mwaka 2017.

Wakili wa kiongozi huyo, Zibusiso Ncube alisema mteja wake alitoweka baada ya kuhofia kukamatwa na kuwekewa sumu.

Wakili Ncube alisema mteja wake alikuwa tayari kujibu maswali lakini aliondoka aliposikia polisi walikuwa na maagizo ya kumtia kizuizini.

Kiongozi huyo pia alifanya kazi pamoja na Rais wa sasa Emmerson Mnangagwa.

Inaelezwa kuwa makamu huyo alikuwa sehemu ya kikundi ambacho kilitaka Neema ambaye ni mke wa Rais Mugabe afanikiwe badala ya Mnangagwa.

Gazeti la Guardian la Zimbambwe limeripoti kuwa tume hiyo ya rushwa ilitaka kumuhoji kiongozi huyo juu ya madai ya unyanyasaji wa ofisi.

Mapema mwezi huu, Rais Mnangagwa alitangaza kumuachisha kazi Waziri wa Utalii, Prisca Mupfumira kufuatia tuhuma za kutoweka na mamilioni ya dola kutoka katika Mfuko wa Pensheni wa nchi hiyo.

ZACC inadai kwamba fedha hizo zilipotea wakati kiongozi huyo akiwa Waziri wa Kazi na ustawi wa jamii.

Wakati hayo yakiendelea Rais Mugabe amelazwa nchini Singapore kwa zaidi ya miezi minne sasa. Agosti 6 Rais Mnangagwa alilitangazia Taifa hilo kwamba kiongozi huyo alipelekwa nchi Singapore kwa ajili ya matibabu baada ya hali yake kubadilika ghafla.

Mugabe aliong’olewa madarakani katika mapinduzi baridi yaliyofanywa na jeshi mwaka 2017 na baadaye aliyekuwa makamu wake wa Rais, Mnangagwa kuapishwa kuwa Rais wa Taifa hilo.