Ambao hamjasajili laini za simu msimamo wa Serikali ya Tanzania uko palepale

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwele

Muktasari:

Serikali yashikilia msimamo wa kufunga laini zisizosajiliwa Desemba 31 wakati ikisaini makubalino ya ujenzi wa jengo la Umoja wa Posta Afrika (PAPU)

Dar es Salaam. Serikali imesisitiza kuwa Desemba 31, mwaka huu itafunga laini zote za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole na haitaongeza muda wa ziada kwa ajili ya zoezi hilo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwele ameyasema hayo leo wakati wa hafla ya uwekaji saini makubaliano ya ujenzi wa jengo la ofisi ya Umoja  Posta Afrika litakojengwa jijini Arusha.

Amesema, “Tarehe 31 tunakamilisha usajili tutakata laini zote ambazo zitakuwa  hazisajiliwa,naomba tu niwaambie umuhimu wa hili zoezi, tumefanya hivi kwa sababu watanzania wengi wanaibiwa mtu mmoja anakuwa na laini 100 na kuanza kufanya uhalifu.”

Akizungumzia ujenzi wa jengo hilo litakalogharimu Sh33.5 bilioni, Waziri Kamwelwe  amesema litajengwa kwa ushirikiano kati ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)    na Umoja wa Posta Afrika(PAPU).

Shughuli ya utiaji wa saini hizo umefanywa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA,  Mhandisi James Kilaba na Mkuu wa Operesheni, Teknolojia wa PAPU, Nathan Mkandawile  na  mkandarasi kutoka China  wa kampuni ya Beijing Contruction Company Limited.

Kamwelwe  amesema   umoja huo ambao unashirikisha nchi 45 za Afrika,  umekubaliana kujenga jengo hilo jijini Arusha ambako  kutakuwa makao makuu.

Amesema  kutokana na umuhimu wa jengo hilo, Serikali itatoa ushirikiano ili kuhakikisha linajengwa kwa ubunifu na ustadi mkubwa na kwa kuanzia Serikali imetangaza kutoa msamaha wa kodi  kwa vifaa vyote vitakavyotumika kwa ajili ya ujenzi.

“Ni  mradi wenye hadhi kubwa kwa Taifa na Kimataifa ,serikali  itasimamia kuhakikisha  ujenzi huu unakuwa na ubora  na ufanisi mkubwa  na unapaswa ukamilike chini ya kipindi  cha miaka miwili(miezi 24) unatakiwa uwe umekwisha pamoja na mkanadarasi kupewa miezi 30,”alisema Mhandisi Kamwelwe.

Amebainisha kuwa  kwakuwa serikali ipo nyuma ya mradi huo uangalizi utakuwa mkubwa kwakuwa awali ulishindwa kutekelezeka baada   ya kuwapo kwa ukwamishaji kutoka kwa  baadhi ya nchi wanachama.

Mhandisi Kilaba h  amesema mradi huo ulisainiwa  tangu Septemba 2016 lakini uwepo wa vikwazo kutoka katika baadhi ya nchi wanachama umefanya ujenzi huo kuchelewa.

“Ujenzi wa mradi huu ulikuwa  na mziengwe mingi lakini kwa sasa mpaka tumefikia hatua yakusaini maana yake  tumeweza kushinda vikwazo hivi vya kisiasa ambavyo tuliwekewa na baadhi ya  nchi,” alisema Mhandisi Kilaba.