Anayepumulia mashine afungiwa umeme, alia na gari la wagonjwa

Muktasari:

Licha ya Hospitali ya Muhimbili tawi la Mloganzila kutoa ahadi ya vipimo bure kwa mgonjwa anayepumulia mashine Hamadi Awadh, mpaka leo mgonjwa huyo ameshindwa kwenda kufanyiwa vipimo upya kutokana na kukosa gari la wagonjwa (ambulance) kwa ajili ya kwenda kufanyiwa uchunguzi wa matibabu hospitalini hapo.


Dar es Salaam. Baada ya kufanikiwa kufungiwa umeme na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mgonjwa anayepumulia mashine, Hamadi Awadh (28) amekwama kufika Hospitali ya Mloganzila, Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya yake.

Uchunguzi huo unatarajia kutoa majibu iwapo mgonjwa huyo anaweza kuendelea na matibabu nje ya Tanzania.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Septemba 10,2019 nyumbani kwake Kipawa Dar es Salaam, Awadh amesema anashindwa kutoa taarifa sahihi kwa Watanzania wanaohitaji kumsaidia kutokana na kushindwa kujua kuhusu matibabu yake ya baadaye.

"Mloganzila wameniambia niende kufanyiwa uchunguzi upya na jopo la madaktari wangu, lakini nimekwama na sijui itakuwaje mtungi huu (anauonyesha) hauwezi kuingia kwenye gari, sina namna ya kufika, nawaomba wanitumie ambulance (gari la wagonjwa) yenye mtungi mdogo au hospitali yoyote inisaidie niweze kufika," amesema Awadh na kuongeza iwapo ambulance ingekuwa ya kukodi angelifanya hivyo.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili tawi la Mloganzila, Dk Julieth Magandi amesema kuwa jopo la madaktari limekubaliana kumfanyia uchunguzi upya Awadh ili kujiridhisha kuhusu matibabu yake ya mwendelezo, lakini anatakiwa atafute usafiri wa kumfikisha hospitalini hapo.

Kuhusu umeme, Awadh aliomba msaada baada ya kushindwa kumudu gharama za malipo ya umeme baada ya mashine anayopumulia kutumia umeme za zaidi ya Sh50,000 kwa wiki.

Septemba 5,2019 Tanesco ilipokea maombi hayo na kumchangia kiasi cha Sh11.5 milioni, Sh1.5 milioni ikiwa ni gharama ya umeme kwa miezi sita na Sh10 milioni ikiwa ni fedha za matibabu nje ya nchi.

Septemba 7 na 8, 2019 mafundi kutokana Tanesco walifanikiwa kufunga umeme nyumbani kwa Awadh na sasa ameanza kutumia vifaa vingine vya umeme ikiwemo feni, friji, Televisheni na redio ambavyo awali hakuweza kuvitumia ikiwa ni sehemu ya kupunguza gharama.