Asasi za Kiraia zachangia mabilioni ya fedha uchumi wa Tanzania

Tuesday November 5 2019

 

By Rachel Chibwete, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza Afrika Mashariki, Aidan Eyakuze amesema asasi 16 zisizokuwa za kiserikali zimechangia Sh236 bilioni kwenye uchumi wa Taifa.

Amesema kati ya fedha hizo, Sh169 bilioni zimetumika nchini kwa ajili ya wanufaika mbalimbali pamoja na watoa huduma kwa umma.

Eyakuze ametoa kauli hiyo leo Jumanne Novemba 5, 2019 Jijini hapa wakati akiwasilisha mada katika Kongamano la Azaki linalofanyika  jijini hapa na kuzikutanisha zaidi ya azaki 500.

“Kati ya fedha hizo, Sh45 bilioni zimetumika kwa ajili ya kuwalipa waajiriwa mbalimbali hasa mishahara au ujira na mafao kwa wastahiki mbalimbali,” amesema Eyakuze.

Amesema kati yake fedha hizo, Sh19 bilioni  zilitolewa serikalini kwa ajili ya kulipia kodi, ushuru na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kodi nyingine zinazotakiwa kulipwa serikalini.

“Pia, kati ya fedha hizo, Sh3 bilioni zilitumika kama akiba ya ustawi na mustakabali wa uendeshaji asasi hizo za kiraia nchini. Kwa takwimu hizo inaonesha wazi Azaki zina mchango mkubwa katika kujenga uchumi nchini,” amesema Eyakuze.

Advertisement

Akilinganisha na huduma nyingine, Mkurugenzi huyo amesema fedha hizo Sh236 bilioni ni sawa na kilo 2,181 za dhahabu zinazosafirishwa kwenda nje, au sawa na watalii 42,316 kukaa nchini kwa wiki moja au lita 247 milioni za petroli, dizeli na mafuta ya taa.

“Pia fedha za kodi Sh19 bilioni ni sawa na mapato yatokanayo na maji ya kunywa, vinywaji laini na sigara ambayo yanafikia sh 18.8 bilioni kwa hesabu za mwaka 2018/19.

“Lakini pia ni sawa na kodi ya serikali iliyokusanywa katika mikoa ya Rukwa, Lindi, Simiyu, Songwe na Katavi kwa pamoja katika mwaka 2018/19 ambayo ni sh bilioni 21.” Amesema.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS), Francis Kiwanga amesema lengo la kongamano hilo ni kuleta pamoja wadau ziadi ya 500 wa asasi za kiraia, wabia wa maendeleo na serikali ili kujadili na kuangalia mchango wa asasi katika kujenga uchumi wa nchi.

 

“Lengo ni kuhakikisha kwamba kazi zinazofanywa na Azaki nchini zinatambuliwa na serikali kutokana na mchango wake katika kusaidia jamii kupata huduma kupitia miradi mbalimbali kwenye sekta za afya, elimu, miundombinu na nyingine,” amesema.

 

Mwisho

Advertisement