Asilimia 60 ya vifo Afrika vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza, unene watajwa kuwa tatizo

Muktasari:

Imani ya Waafrika kuwa unene ni afya ni potofu na badala yake imebainika ni chanzo cha magonjwa yasiyoambukiza

Kampala, Uganda. Wadau wa masuala ya afya barani Afrika wameonya kuwa tabia ya Waafrika kudhani maumbo makubwa na unene ni afya imewaweka rehani ya kupata magonjwa yasiyoambukiza mara tatu zaidi ikilinganishwa na mataifa mengine.

Wakati ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2010 ikionyesha kuwa asilimia 47 ya watu 100 hufariki kutokana na magonjwa hayo, dunia inatarajia vifo 60  kati ya 100 vitatokana na magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) ifikapo mwaka 2020.

Hayo yamezungumzwa na wadau mbalimbali wa masuala ya afya jijini Kampala Machi 20 mwaka huu wakati wa kongamano lililojadili afya kwa wote lililojikita zaidi kuzungumzia magonjwa yasiyoambukiza.

Akifafanua kuhusiana na suala la magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) ambayo ndiyo kiini cha mjadala huo, mkurugenzi wa kitengo cha magonjwa yasiyoambukiza kutoka wizara ya afya Uganda, Dk Gerald Mutungi amesema Waafrika wengi wanadhani unene ni sifa na si ugonjwa.

“Nchini Uganda na maeneo mengi barani Afrika unene ni ufahari, unaonekana kama ni tajiri na unayafurahia maisha ya kwamba umefanikiwa. Watu wanapewa majina kama ‘boss’ na kuonekana maisha kwao hayawapi shida,” amesema.

Amesema wengi wanapenda kutumia vyombo vya moto wakati wote kuendeshwa na kuendesha magari, kupanda pikipiki mpaka mlangoni na kama ingewezekana watu wangeendeshwa mpaka vyooni. “Tunahitaji kuitumia miili yetu zaidi kama ambavyo baba zetu waliitumia zamani.”

Amesema mtu mmoja kati ya wanne nchini Uganda ana shinikizo la damu na hajui kuhusu hali yake kiafya.

“Na asilimia nne ya watu wazima nchini Uganda wana kisukari wakati asilimia 80 hawajui kama wana hali hiyo na asilimia 40 ya vifo nchini humo vinachangiwa na magonjwa yasiyoambukiza,” amesema Dk Mutungi.

Hata hivyo nchini Tanzania, taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (Nimr) imekuwa ikifanya kazi na Serikali kwa kushirikiana na WHO katika tafiti za uchunguzi ambazo zimeonyesha kuwa kasi ya kukua kwa magonjwa yasiyoambukiza ipo juu.

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa, watumiaji wa tumbaku Tanzania ni asilimia 15.9, watumiaji wa pombe asilimia 29.3, wenye uzito mkubwa na wanene asilimia 34.7, wenye lehemu  mwilini asilimia 26 na wanye mafuta mengi asilimia 33.8.

Lakini pia zimeonyesha kuenea kwa kasi kwa ugonjwa wa kisukari kwa asilimia 9.1 na shinikizo la damu kwa asilimia 25.9.

Utafiti  wa WHO umeonyesha kuwa, vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukiza vitaongezeka kwa asilimia 15 duniani kati ya mwaka 2010 na 2020 kutoka 36 mpaka kufikia milioni 44. Ongezeko la juu linatarajiwa kutokea katika nchi za Afrika.

Mwaka 2010, WHO ilitoa utafiti ulioitwa ‘Global status report on non-communicable diseases’  uliozungumzia hali ya magonjwa yasiyoambukiza duniani kote ukionyesha namna magonjwa hayo yanavyosumbua duniani.

Umeonyesha asilimia 47 ya wagonjwa kote duniani walikuwa wakisumbuliwa na magonjwa hayo, huku vifo 100 kati yake 60 vikitokana na magonjwa yasiyoambukiza.

Katika mambo yaliyoibua mjadala zaidi katika kongamano hilo ni pamoja na kuendeleza teknolojia ya kidijitali katika utoaji wa huduma za afya zenye viwango.

Pia suala la muundo wa usambazaji na manunuzi yatakayosababisha upatikanaji wa dawa zenye viwango bora na kwa bei rahisi.

Sauti za wagonjwa na asasi za kiraia katika haki za kupata huduma bora, pamoja na kuchambua vitu muhimu, matatizo na changamoto katika upatikanaji wa fedha kuchangia huduma za afya kwa wasiojiweza.

Mjadala uliochukua nafasi kubwa zaidi ilikuwa ni kuhusu ushirikiano wa sekta binafsi na sekta ya umma katika kutoa huduma za afya kuelekea utekelezaji wa huduma za afya kwa wote UHC.

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Amref Health Africa, Dk Githinji Gitahi amesema viongozi wa mataifa ya Afrika wanapaswa kutambua kuwa hawawezi kuwa na nchi yenye uchumi wa kati kama nchi zao zitakuwa na watu wagonjwa.

“Viongozi wanapaswa kuwekeza katika afya za watu wanaowaongoza, suala hili si la kuchagua ni lazima, kwani huwezi kujenga nchi ikafikia uchumi unaoutarajia kama litakuwa taifa la wagonjwa ni wakati sasa kuwekeza katika afya kwa wote ili kufikia malengo endelevu,” anasema Dk Gitahi.

Hali ilivyo nchini kwa sasa

Akizungumza wakati wa Jukwaa la Fikra la Mwananchi lililofanyika Juni 28 mwaka jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alielezea kwa kina mikakati ya Serikali na mipango ya kisera katika kukabiliana na magonjwa hayo.

Alisema takwimu za WHO mwaka 2010 zinaonyesha endapo hatua mahususi hazitachukuliwa za kupambana na kudhibiti magonjwa hayo,  ifikapo mwaka 2020 takwimu zitapanda kutoka asilimia 47 mpaka asilimia 60 na kwenye vifo itapanda kutoka asilimia 60 mpaka asilimia 73.

“Hapa nchini tunapata picha ya hali ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza kupitia utafiti ulifanywa katika mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Mara na Kilimanjaro miaka ya 1990, lakini naomba nisiende huko, kwa sasa tunatumia utafiti wa Nimr wa mwaka 2012 na ndiyo ambao tunautumia mpaka leo uliofanywa kwa kushirikiana na WHO, wizara ya afya na wadau ule ndiyo unatupatia muhtasari wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza nchini,” amesema.

Amesema mwaka 2016 Serikali ilitengeneza na kuzindua mkakati wa taifa wa kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza wa miaka mitano, ambao umeonyesha maeneo mahususi ambayo yatayafanyia kazi.

“Na eneo kubwa ambalo tulianza nalo ni kutoa elimu kwa umma kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwamo kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi,” amesema.

Akizungumzia Serikali kuepuka gharama kubwa katika kutibu magonjwa hayo, amesema kwa kuwa kisababishi kikubwa ni matumizi ya tumbaku na pombe kupita kiasi, lakini pia suala la mtindo wa maisha.

“Ulaji usiofaa pia ni tatizo kwa mujibu wa tafiti ambapo asilimia 97 ya Watanzania waliohojiwa iwapo wanakula mbogamboga na matunda zaidi ya mara tano kwa siku, asilimia 2.5 tu ndiyo walisema wanakula wengi hawali lakini wataalamu wanaagiza hivyo,” amesema waziri huyo.