Askari Polisi kortini akituhumiwa kuomba rushwa ya Sh200,000

Muktasari:

Watu wawili akiwemo askari polisi ambaye ni mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, Leslie Koini amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kosa la kuomba rushwa ya Sh200, 000.

Dar es Salaam. Watu wawili akiwamo askari polisi ambaye ni mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam nchini Tanzania, Leslie Koini wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu wakikabiliwa na kosa la kuomba rushwa ya Sh200, 000.

Pia,  upande wa mashtaka umedai mshtakiwa ambaye ni karani wa mahakama hiyo Itialy Omary hakuwepo mahakamani hapo hivyo wameiomba mahakama hiyo hati ya kukamatwa mshtakiwa huyo.

Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Odessa Horombe akisoma hati ya mashtaka leo Jumatatu Novemba 18, 2019 amedai washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kupokea rushwa.

Amedai Mei 8, 2018 mshtakiwa Koini akiwa askari polisi kama mwendesha mashtaka na Omary akiwa karani wa mahakama hiyo kwa pamoja walipokea rushwa ya Sh200, 000 kwa Musa Abdallah ikiwa kishawishi cha kumsaidia kukwepa hatia kwenye kesi ya usalama barabarani namba 211/2018 iliyopo katika mahakama hiyo.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa alikiri kosa linalomkabili ambapo Horombe alidai kwa kuwa mshtakiwa amekiri shtaka linalomkabili hivyo bado hajaandaa maelezo ya kosa hilo.

"Naiomba mahakama hii iahirishe shauri hili hadi nikaandae maelezo ya kosa linalomkabili mshtakiwa," alidai Horombe.

Pia, ameieleza mahakama hiyo itoe hati ya kukamatwa kwa mshitakiwa wa kwanza (Omary) ambaye hayupo mahakamani.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Mbando amesema mshtakiwa huyo anatakiwa kuwa na mdhamini mmoja ambaye mwenye vitambulisho vinavyotambulika na atasaini bondi ya Sh500, 000.

Baada ya kutolewa dhamana hiyo mshtakiwa alitimiza masharti hayo na yupo nje kwa dhamana. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 21, 2019.