VIDEO: Auawa akijaribu kumpora Padri Dar

Friday September 6 2019

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mtu mmoja anayedhaniwa kuwa jambazi ameuawa kwa kupigwa risasi baada ya kufanya jaribio la kumpora Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Theresa illiyopo Mbezi jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.

Mwananchi limefika katika kanisa hilo na kukuta walinzi wakiendelea na kazi zao. Hata hivyo, Paroko huyo ambaye jina lake halikutambuliwa, hakutaka kuzungumza na waandishi wa habari.

Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi kampuni ya ulinzi ya Jatu, Jacob Mgwabati amesema tukio hilo limetokea leo Ijumaa Septemba 6, 2019 saa 6 mchana wakati Padri huyo alipofika kanisani akitokea benki.

“Walipofika hapo waka mbana paroko, alikuwa ametokea benki kulipa wafanyakazi, lakini hakuwa na hela. Wakamwambia tupe begi, wakati bado wanashangaa,  wakatoa bastola mbili kila mmoja na bastola yake,” amesema Mgwabati.

“Paroko akaamua kuwapa begi, askari wetu akatumia busara, akaacha kwanza paroko asogee, walipoondoka akawatandika risasi, mmoja ikampata kwenye kiuno akaanguka, hakukaa sana akafa. Huyo mwingine alikimbia kwa miguu.”

Amesema baada ya tukio hilo polisi walioko karibu na kanisa hilo walifika na kumkagua mtu huyo na kumkuta na vitambulisho mbalimbali na leseni ya udereva na hirizi.

Advertisement

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mussa Taibu amekiri kulifahamu tukio hilo akisema mlinzi wa kampuni ya Jatu amefanya kazi nzuri.

“Ni kweli, kuna mchungaji alikuwa ameingia benki, ile ametoka tu wakajua ana hela, sasa wakajitokeza pikipiki mbili sasa pale palikuwa na ulinzi. Wale majambazi wakatoa bastola huku na huku.”

Amesema kwa sasa bado wanafanya uchunguzi na wanaendelea kumtafuta mtu mwingine aliyekimbia katika tukio hilo.

 

Advertisement