Awamu ya pili ya vita yaanza, JWTZ yaingia Uganda-11

Mmoja wa makamanda hodari wa Vita vya Kagera, Brigedia John Bulter Walden a.k.a Black Mamba

Muktasari:

Jana tuliona Mwalimu Nyerere alipokabiliwa na Nchi Huru za Afrika (OAU) pamoja na mataifa kadhaa wakimtaka asitishe vita dhidi ya Uganda, alitoa masharti matatu. Moja, OAU imkemee Idi Amin kwa kitendo chake cha uvamizi. Pili, Idi Amin aahidi na

akane kwamba hataki sehemu yoyote ya Tanzania. Na tatu, Amin aahidi kulipa fidia kwa uharibifu alioufanya. OAU haikumkemea Amin, Nyerere akaamuru JWTZ iingie Uganda kumng’oa. Hapo ndipo awamu ya pili ya Vita vya Kagera ilipoanzia. Sasa endelea

Kuingia ndani ya Uganda ilikuwa ni awamu ya pili ya Vita vya Kagera. Kabla awamu hiyo haijaanza, kulifanyika mabadiliko ya uongozi kwenye uwanja wa vita. Baada ya kufanya kazi kwa muda wa miezi mitatu akiwapanga wapiganaji wa JWTZ na kuirejesha ardhi ya Tanzania iliyotekwa na Idi Amin, Brigedia Jenerali Tumainieli Kiwelu alirejeshwa Dar es Salaam. Kazi ya kuingia Uganda ikaenda mikononi mwa kamanda mwingine, Meja Jenerali David Msuguri.

Ilipangwa miji ambayo ingeanza kutekwa ambayo ni Masaka na Mbarara. Hii ikabatizwa jina la Mapigano ya Masaka ambayo ilidumu kwa siku mbili tu; Ijumaa na Jumamosi ya Februari 23 na 24, 1979 na ikamalizika.

Lakini kabla Masaka haijafikiwa kulikuwa na miji midogo midogo ya kutekwa. Mmojawapo ni Lukoma ambako kuna uwanja mdogo wa ndege uliojengwa mahsusi kwa shughuli za kivita na ni umbali wa kilomita 20 kutoka mpaka wa Tanzania.

Ndege za kijeshi zilizoishambulia Tanzania zilipaa kutoka katika uwanja huo uliozungukwa na vilima vya Nsambya, Kikandwa na Simba. Vilima vyote hivi askari wa Idi Amin walikuwa wametanda wakiwa na silaha kali za kivita vikiwamo vifaru na mizinga mikubwa.

Brigedi tatu zilizokamilika 201, 207 na 208 zilitumwa kuingia Masaka. Mpango wa awali ulikuwa ni kuzitumia brigedi za 201 na 208 kushambilia vilima vya Simba kutokea Kusini-Magharibi na Brigedi ya 207 ishambulie kutokea Mashariki.

Lakini baadaye taarifa za kiintelijensia zilisema kulikuwa na zaidi ya askari 500 wa Idi Amin wakiwa na vifaru na mizinga mikubwa eneo la Katera kwenye rasi ya Sango Bay, eneo la Kakuuto upande wa pili wa Ziwa Victoria. Kuwaacha hawa ingefanya eneo la upande huo wa Tanzania kuwa hatarini zaidi kushambuliwa.

Kwa hiyo iliamuliwa Brigedi ya 207 ianze kushambulia Katera. Kulikuwa na njia mbili za kufika Katera kutokea Minziro. Njia ya kwanza na rahisi zaidi ilikuwa ni barabara kuu, lakini kwa kutumia njia hiyo jeshi la Tanzania lingekutana na mashambulizi ya uso kwa uso kutoka jeshi la Idi Amin.

Njia ya pili na ngumu zaidi ni kupita kwenye uchochoro wenye mabwawa yaliyojaa maji kutokana na mvua iliyokuwa ikinyesha. Huu ni upande wa pili wa Ziwa Victoria.

Askari wachache waliozaliwa katika vijiji vilivyozunguka ziwa karibu na Bukoba na ambao walijua lugha na tamaduni za eneo hilo walichaguliwa wasonge mbele, wakivalia nguo za kiraia na kubeba matairi ya baiskeli na bidhaa nyingine kama vile wanakwenda sokoni. Askari waliobaki nyuma wakawafuatilia kwa kufuata nyayo zao.

Siku iliyofuata walirudi wakiwa wamechoka kupita kiasi na wengine wakiwa wagonjwa. Waliripoti kuwa mvua kubwa iliyonyesha iliharibu sana barabara kiasi cha kutopitika.

Pamoja na ripoti ya wanajeshi hao, Kamanda wa brigedi hiyo, Brigedia John Butler Walden, aliamua ni lazima wasonge mbele hata kama hali ya hewa ni mbaya kiasi gani. Huyu ni brigedia aliyeitwa ‘Black Mamba’.

Kwa kuwa alijua wanajeshi wake wasingepata moyo wa kusonga mbele bila yeye kwenda nao bega kwa bega, aliamua kutembea nao kwa mwendo wa zaidi ya kilomita nane za kwanza kutoka Minziro hadi kilima cha Bulembe.

Brigedia Walden alidhani mwendo kwa hizo kilomita nane ungewachukua saa chache kupita kwenye msitu mnene, lakini iliwachukua karibu saa 11 wakipambana na matope, madimbwi makubwa ya maji, mbu na mbung’o na maeneo mengine walilazimika kutembea kwenye madimbwi ya maji yaliyowafika mabegani karibu kabisa na kuzama.

Hatimaye walipofika eneo ambalo lilikuwa kavu kwa kiasi fulani, Brigedi ya 207 ilipumzika kidogo kisha ikaanza tena matembezi marefu kuelekea Kaskazini umbali wa kilomita 28 kuingia ndani ya Uganda katika mji wa Katera.

Walipodhani masaibu yamekwisha, ndipo yalipoongezeka. Wadudu kama mbu na mbung’o wakaongezeka. Brigedi ya 207 ikajikuta katika vita ya aina mbili kupambana na jeshi la Idi Amin na wadudu wanaokera katika msitu mnene, huku mvua ikinyesha na barabara yenye madimbwi kujaa maji.

Silaha walizokuwa nazo zikalowa maji. Kutokana na barabara kutopitika kwa gari hata zile gari za jeshi askari wa brigedi hii walilazimika kubeba vichwani mwao silaha zao na zana zingine za kivita.

Hatari kubwa zaidi kuliko mbu na mbung’o ilikuwa ni wanyama kama mamba na viboko waliokuwa maeneo hayo, hususan kuelekea Sango Bay. Kwa hiyo kulikuwa na hofu nyingine ya wanajeshi hao kushambuliwa na hata kuliwa na wanyama hao wakali.

Kwa umbali wa kilomita 28, na kutokana na ubovu mkubwa wa njia waliyopita ikiwa na madimbwi makubwa yaliyojaa maji, ikijumlishwa na mashambulizi ya wadudu, brigedi hiyo ilitumia muda wa saa zaidi ya 50 bila kupumzika wala kula.

Redio za mawasiliano walizokuwa nazo zililowa maji hata zikashindwa kufanya kazi. Kwa hiyo walipoteza mawasiliano kabisa na makao makuu ya kikosi chao.

JWTZ ilianza kuwatafuta wanajeshi hao bila mafanikio. Kukawa na hofu kubwa kuwa Brigedi ya 207 imeshambuliwa na kufyekwa yote. Hakukuwapo na namna yoyote ambayo yeyote katika brigedi hiyo angeweza kufikiwa.

Hatimaye ilipofika saa 11 jioni ya siku ya tatu, brigedi hiyo ikaibuka kutoka kwenye mabwawa ya maji na matope. Angalau sasa redio zikaanza kufanya kazi na wakaweza kuwasiliana na kituo chao cha kazi.

Ingawa hakuna mwanajeshi hata mmoja aliyepoteza maisha, zaidi ya 200 miongoni mwao walikuwa wagonjwa na wachovu mno kiasi kwamba walishindwa kusonga mbele. Wengine walifikia hatua ya kushindwa hata kutembea kiasi kwamba ilitumwa helikopta ya jeshi kuwabeba.

Kwa kuwa wanajeshi wa JWTZ walikuwa wamechoka sana, iliamuliwa kuwa wasubiri hadi kupambazuke ndipo mashambulizi yaanze. Je, walianza kushambulia? Na walishambuliaje?

Itaendelea kesho