Baada ya kina Lugola, wengine sita kuhojiwa leo

Waliokuwa wajumbe 6 wa kamati ya utekelezaji wa makubaliano iliyosainiwa Agosti 22,2019 kati ya jeshi la zimamoto na ukoaji pamoja na kampuni ya Rom Solutions Co. Ltd wakiwa katika ofisi za Takukuru makao makuu kwa ajili ya kuhojiwa. Picha na Nazael Mkiramweni

Muktasari:

Watu sita ambao walikuwa wajumbe wa kamati ya  utekelezaji wa makubaliano iliyosainiwa Agosti 22, 2019 kati ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kampuni ya Rom Solutions Co Ltd wamefika ofisi za Takukuru kuhojiwa.

Dodoma. Watu sita ambao walikuwa wajumbe wa kamati ya  utekelezaji wa makubaliano iliyosainiwa Agosti 22, 2019 kati ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kampuni ya Rom Solutions Co Ltd wamefika ofisi za Takukuru kuhojiwa.

Wamefika katika ofisi za taasisi hiyo ya kuzuia na kupambana na rushwa mjini Dodoma nchini Tanzania leo Jumatano Februari 5, 2020.

Kuhojiwa kwa watu hao kumekuja siku chache baada ya Takukuru kuwahoji watu watano, akiwemo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola.

Wengine waliohojiwa ni naibu waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni; naibu katibu mkuu wa wizara hiyo, Ramadhani Kairima; aliyekuwa mkuu wa jeshi hilo, Kamishna Jenerali Thobias Andengenye na aliyekuwa katibu mkuu, Meja Jenerali Jacob Kingu ambaye alijiuzulu na baadaye kuteuliwa kuwa balozi.

Wanahojiwa kutokana na agizo la Rais John Magufuli baada ya kuwataja kuhusika katika mkataba kati ya Jeshi la Zimamoto na kampuni hiyo   kwa ajili ya kununua vifaa mbalimbali vya kuzima moto.

Kufuatia tuhuma hizo, Magufuli alitengua uteuzi wa Lugola  na Andengenye na kuagiza wote waliohusika kuhojiwa na Takukuru.

Wajumbe hao wanadaiwa walipewa kompyuta mpakato na  Dola 800 za Kimarekani kama posho za vikao.

Waliofika Takukuru leo ni Kamishna wa Zimamoto, Mbaraka Semwanza; Fikiri Salla, Lusekelo Chaula, Ully Mburuko (wote naibu kamishna wa jeshi hilo); mchumi mkuu wa Zimamoto,  Boniphace Kipomela na Felis Mshana ambaye ni mchumi wa jeshi hilo.

Wajumbe hao waliingia Takukuru kwa nyakati tofauti huku kila mmoja akikaguliwa kabla ya kupita getini.

Wakati wakiingia, walikuwa wamebeba kompyuta mpakato kasoro mjumbe mmoja.