Baada ya ndugu kumsaka kwa siku nne, Polisi yakiri kumshikilia kiongozi Chadema

Tarime/Mwanza. Jeshi la Polisi limekiri kumshikilia kiongozi wa Chadema wilayani Tarime, kwa uchunguzi kuhusiana na tuhuma mbalimbali.

Kauli hiyo imekuja baada ya jeshi hilo kukana kwa siku nne mfululizo kujua alipo.

Akizungumza kwa simu jana, Kamanda wa Polisi mkoa wa kipolisi Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe alisema kiongozi huyo, Matibwi Magoiga anashikiliwa tangu Mei 15.

“Anahojiwa kwa tuhuma mbalimbali miongoni mwa tuhuma hizo ni kuhusiana na mapigano ya koo,” alisema Mwaibambe bila kufafanua.

Alipoulizwa sababu za kukana kumshikilia mtuhumiwa huyo kwa kipindi chote hicho, kamanda Mwaibambe alisema polisi inao utaratibu wake wa kufanya kazi.

Hatua ya Polisi kukiri kumshikilia Magoiga ambaye ni katibu wa Chedema Kata ya Nyarero, kumemaliza wingu la hofu na sintofahamu iliyoikumba familia yake tangu alipochukuliwa nyumbani kwake na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi.

Hofu hiyo ilitokana na kukwama kwa jitihada za familia, ndugu na viongozi wa chama chake za kumtafuta katika vituo vya polisi wilayani humo baada ya polisi kukana kumshikilia wala kujua alipo.

Pamoja na Magoiga, watu hao waliojitambulisha kuwa askari polisi waliwakamata na watu wengine watatu waliotajwa kwa majina ya Mwita Mgesi, Charles Magige na Inchota Mchuma.

Watu hao wengine waliochukuliwa kwenye nyumba zao kati ya saa 6:00 hadi 6:30 usiku wa kuamkia Mei 15, walishikiliwa katika Kituo cha Polisi Borega, wilayani Tarime.

Katibu wa Chadema Jimbo la Tarime Vijijini, Sunday Magacha aliyekuwa miongoni mwa viongozi wa chama hicho walioshirikiana na ndugu kumtafuta Magoiga alisema, “tulizunguka vituo vyote vya polisi wilayani Tarime kumtafuta Magoiga bila mafanikio; polisi walikana kumshikilia wala kujua alipo.”

Katibu wa mbunge wa Tarime Vijijini, Mrimi Zablon alisema baada ya jitihada za viongozi wa Chadema Wilaya ya Tarime kujua alipo Magoiga kushindikana, waliomba msaada kwa mbunge, John Heche ambaye pia alijibiwa na uongozi wa Polisi kuwa hawamshikilii.

Kamanda Mwaibambe alisema uchunguzi wa kina unaendelea kuhusu tuhuma dhidi ya Magoiga na ushahidi ukipatikana atafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

“Tukikamilisha upelelezi tutamfikisha mahakamani kesho (leo) au keshokutwa (kesho) kutegemea na ushahidi,” alisema.