Baba aeleza mauaji ya mwanaye yalivyokatisha ndoto kuwa muuguzi

Wednesday October 23 2019

 

By Joyce Joliga, Mwananchi [email protected]

Songea. Christopher Kafuru ambaye ni baba wa Beata Kafuru anayedaiwa kuuawa na mpenzi wake amesema mwanaye amekatishwa ndoto ya kuwa muuguzi.

Amesema haki inatakiwa kutendeka ili ukweli kuhusu kifo hicho ujulikane na mhusika kuchukuliwa hatua.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani Ruvuma, Simon Maigwa, mtuhumiwa alichukua uamuzi huo baada ya kumtuhumu Beata kuwa na uhusiano wa mapenzi na mtu mwingine.

Beata anadaiwa kuuawa na James Paul ambaye ni ofisa wa Takukuru Oktoba 20, 2019 wilayani Tunduru kwa kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.

Katika ufafanuzi wake Kamanda Maigwa amesema  mtuhumiwa alikiri kufanya mauaji hayo kwa lengo la kulipiza kisasi na alitumia bastola aina ya Browning na kumpiga  Beata risasi tatu za kichwani ambaye alikufa hapo hapo.

Akizungumza na Mwananchi, Kafuru amesema, “hadi sasa nakosa cha kuzungumza, Beata ni mtoto wangu wa pili kati ya watoto wangu wanne. Ningejua kama anakwenda kukatishwa uhai ningemzuia asirudi Tunduru kuripoti kazini, ningemshauri kuacha kazi.”

Advertisement

“Alikuwa na ndoto za kuwa muuguzi kama dada yake, alipanga kusoma shahada ya uuguzi.”

Amesema Beata baada ya kumaliza masomo stashahada  ya uuguzi Oktoba, 2019 alikwenda Mbozi kuwasalimia wazazi wake, aliporejea kazini aliuawa.

“Alipokuwa mapumziko alinieleza vitu vingi, alinieleza jinsi ambavyo hawakuwa na maelewano nikamtaka wakae na kuzungumza. Binti yangu alisoma kwa kutumia mshahara wake, si kweli kwamba alisomeshwa na huyo mwanaume na yeye ndiye aliyekuwa akimsaidia,” amesema.

Amesema mwanaye alikuwa akikataa kusomeshewa na mwanaume ambaye hajafunga naye ndoa.

Advertisement