Barrick: Tutajifunza kwa makosa tuliyofanya Tanzania

Muktasari:

Ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Barrick Gold,  Dk Mark Bristow amesema kampuni hiyo itajifunza kwa makosa iliyoyafanya nchini Tanzania miaka 10 iliyopita

Dar es Salaam. Ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Barrick Gold,  Dk Mark Bristow amesema kampuni hiyo itajifunza kwa makosa iliyoyafanya nchini Tanzania miaka 10 iliyopita.

Dk Bristow ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Januari 24, 2020 Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na kamati ya madini ya Barrick.

“Tukiangalia uzoefu tunayo mengi ya kujifunza kutokana na makosa mengi tuliyofanya huko nyuma. Kama hatutajifunza kwa yaliyopita na kufanya vizuri hatustahili kuwa hapa,” amesema Dk Bristow.

Amesema tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani kumekuwa na safari ndefu ya majadiliano kati ya kampuni hiyo na Serikali yaliyowezesha kugawana mapato sawa.

“Sisi wawekezaji tunapokuja kwenye nchi kama hii tuna jukumu kubwa la kuchimba rasilimali ya Taifa si kwa faida yetu tu bali kwa faida pia ya Taifa na wadau wengine. Wadau hao siyo tu wanahisa, bali wananchi ndiyo maana ni wajibu wetu kulipa kodi.”

“Vilevile siyo tu kwa Watanzania wa sasa bali pia vizazi vijavyo vina haki ya kupata mgawo. Kuna jamii zinazozunguka migodi, lazima zishiriki shughuli za uchumi,” amesema.

Amesema wakati mchakato wa makubaliano ukiendelea, kulikuwa na ukosoaji na maneno mengi ambapo baadhi ya watu walisema ushirikiano huo hautakuwa na faida.

“Watu wengine walikosoa msimamo wako (Rais John Magufuli) kwamba unafukuza wawekezaji lakini tumefikia mahali ambapo kama tunapata,  tunapata wote na kama tunakosa,  tunakosa wote.”

“Afrika tuna tabia ya kulalamika sana kwamba tunapata kidogo, lakini kama tunapata asilimia 50 kwa 50 maana yake tunapata pamoja. Mimi ni Mzulu na nimezaliwa kwa Wazulu, tunao msemo unaosema huwezi kuosha mko mmoja bila mwingine,” amesema Dk Bristow huku akimpa Rais Magufuli.

Baada ya mgogoro uliodumu tangu mwaka 2017, Kampuni ya Barrick na Serikali ziliunda kampuni ya Twiga itakayosimamia migodi mitatu iliyokuwa chini ya kampuni ya Acacia.

Kwenye kampuni hiyo mpya, Barrick itamiliki asilimia 84 ya hisa zote huku Serikali ikiwa na asilimia 16. Utaratibu huo ni utekelezaji wa sheria mpya ya madini iliyopitishwa mwaka 2017.

Mgogoro kati ya Serikali na kampuni ya Acacia iliyokuwa inasimamia migodi ya Buzwagi, North Mara na Bulanhulu ulianza mwaka 2017 na Rais Magufuli akaunda tume ya kuchunguza mwenendo wa biashara ya madini.

Tume hiyo ilibaini ukiukwaji wa sheria, utaratibu na kanuni zilizopo hivyo kuikosesha Serikali mapato inayostahili. Kutokana na hilo, Serikali iliipiga faini ya Dola 190 bilioni jambo lililosababisha kuanza kwa mzungumzo baina ya pande hizo mbili.

Kwenye mazungumzo hayo, Acacia ambayo ni kampuni tanzu ya Barrick iliwekwa pembeni na majadiliano yakafanywa na Barrick, mwisho wa siku, Acacia imefutwa sokoni na badala yake, Twiga itachukua nafasi yake.