Bei mafuta petroli, dizeli yashuka Tanzania

Muktasari:

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Desemba 3, 2019 na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) nchini Tanzania imesema bei ya mafuta ya petroli dizeli na mafuta ya taa zitapungua kuanzia kesho Jumatano Desemba 4, 2019.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) nchini Tanzania imetangaza bei za kikomo kwa bidhaa za mafuta nchini humo zitakazoanza kutumika kuanzia kesho Jumatano Desemba 4, 2019.

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Desemba 3, 2019 kwa vyombo vya habari na kaimu mkurugenzi mkuu wa Ewura, Nzinyangwa Mchany imesema bei za jumla na rejareja za mafuta za petroli dizeli na mafuta ya taa zimepungua.

Mchany amesema mafuta hayo ni yale yaliyoingia kupitia bandari ya Dar es Salaam ambayo yamepungua ukilinganisha na mwezi uliopita.

“Kwa Desemba 2019, bei za rejareja za Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimepungua kwa Shilingi 31/lita (sawa na asilimia 1.39), Shilingi 33/lita (sawa na asilimia 1.52) na Shilingi 43/lita (sawa na asilimia 2.02)” amesema

“Bei za jumla za Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimepungua kwa Shilingi 30.46/lita (sawa na asilimia 1.47) na Shilingi 32.63/lita (sawa na asilimia 1.60) na Shilingi 42.63/lita (sawa na asilimia 2.14)”

Amesema bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli yanayoingizwa nchini kupitia bandari ya Tanga na Mtwara nazo zimepungua ikilinganishwa na mwezi uliopita.

“Punguzo la bei za mafuta katika soko la ndani kwa mafuta yaliyoingizwa nchini kupitia bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara linatokana na kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji (BPS premiums)” amesema