Benki ya DCB yaelezea mafanikio ya ‘Lamba Kwanza’

Mkurugenzi wa Biashara Benki ya Biashara DCB, James Ngaluko (wa pili kutoka kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwisho wa kampeni ya Lamba Kwanza. Picha na Muyonga Jumanne

Muktasari:

Benki ya Biashara ya DCB imezungumzia kampeni yake iliyoanza Mei 2019 hadi Septemba iliyoitwa ‘Lamba Kwanza’ ambayo imeonyesha mafanikio.

Dar es Salaam. Benki ya Biashara ya (DCB) imevuka malengo ya kukusanya amana za Sh18.5 bilioni sawa na asilimia 123 kutoka Sh15 bilioni iliyotarajia katika kampeni ya miezi mitatu iliyoitwa 'Lamba Kwanza' .

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Septemba 24,2019 Mkurugenzi wa Biashara wa benki hiyo, James Ngaluko amesema kampeni hiyo ilianza Mei 2019 na imefika tamati Septemba imewawezesha wateja kupata riba hadi asilimia 14.

"Hadi kampeni inaisha benki imeweza kukusanya Sh18.5 bilioni  ambapo kuna ongezeko la asilimia 23 kutokana na Sh3.5 bilioni iliyoongezeka kwenye lengo la awali la kukusanyaSh15 bilioni," amesema Ngaluko.

Ngaluko amesema licha ya kampeni hiyo kuisha wateja wataendelea kupata bidhaa ya 'Lamba kwanza'.

Ngaluko ameeleza kampeni hiyo imechangia katika mafanikio ya benki hiyo hadi kufikia Juni 2019 ilipata faida ya Sh1.2 bilioni sawa na asilimia 118 kutoka Sh1 bilioni Juni 2018.

"Tumeendelea kupunguza riba kwa mikopo ya ujenzi na ununuaji wa nyumba hadi chini ya asilimia 20 kutoka asilimia 22 na marejesho kutoka miaka 15 hadi miaka 10," amesema Ngaluko.