Bosi ATCL azungumzia Bombardier iliyoharibika

Muktasari:

Mkurugenzi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Ladslaus Matindi amesema ndege aina Bombardier Q400 iliyokuwa katika matengenezo imeanza kufanya safari zake kama kawaida


Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Ladslaus Matindi amesema ndege aina Bombardier Q400 iliyokuwa katika matengenezo imeanza kufanya safari zake kama kawaida.

Ametoa ufafanuzi huo leo Jumatano Agosti  21, 2019 katika kipindi cha Power Breakfast cha Redio Clouds akizungumzia taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zikionyesha picha ya ndege hiyo ikiwa katika matengenezo.

Katika maelezo yake Matindi amesema ndege hiyo ilikuwa na hitilafu na ilitengenezwa kwa siku moja na tayari imerejea katika ratiba zake za safari za kila siku.

“Ndege inaweza kuharibika, kupata hitilafu au kuingiliwa na kitu kutoka nje muda wowote kwakuwa ni mashine hakuna namna ya kuzuia hilo ni jambo la kawaida kwa mashine hata binadamu,” amesema Matindi.

Amesema ndege hiyo ipo Dar es Saalam tangu jana na matengenezo yake yalichukua siku moja, akibainisha kuwa yalianza Jumatatu mchana hadi jana mchana, “Usiku jana iliruka kurudi Dar es Salaam.”

“Ndege zinazoharibika sio za ATCL  pekee bali popote hata KLM ndege zao huwa zinaharibika, British Airways na Emirates wakisema ndege zao hazijawahi kuharibika ndipo tujiulize kwa nini zetu ziharibike.”