Bosi TACAIDS ataka kondomu kugawiwa bure

Muktasari:

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Dk Leonard Maboko ameeleza anavyotamani kushuhudia Serikali ikigawa kondomu bure, hasa katika maeneo hatarishi.


Mwanza. Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Dk Leonard Maboko ameeleza anavyotamani kushuhudia Serikali ikigawa kondomu bure, hasa katika maeneo hatarishi.

Dk Maboko ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Novemba 28, 2019 katika kongamano la kitaifa la maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani lililofanyika jijini Mwanza.

Amesema anatamani mwaka 2020 nyumba zote wageni, baa na maeneo mengine kondomu kugawiwa bure.

Amesema lengo ni kuzuia maambukizi mapya ya Ukimwi kwa vijana kwa maelezo kuwa kwa sasa ndio kundi linaloongoza kwa kupata maambukizi mapya.

"Natamani mwakani tuweze kusambaza kondomu kila mahali ili tuweze kudhibiti ugonjwa huu, najua huko ndiko watu wanakutana na kufanya wanavyofanya lakini  kama Serikali tuone namna gani tunawasaidia wale wanaoshindwa kununua," amesema

Amesema ifike mahali hali ya kuzuia maambukizi isichukuliwe kama mzaha licha ya kupungua kutoka 100,000 hadi 72,000.

Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAIDS), Leo Zekeng amesema mwaka 2018 watu 37 milioni walikuwa wanaishi na virusi vya Ukimwi, 36 milioni wakiwa ni watu wazima na watoto milioni 1.7 walio chini ya miaka 15 ulimwenguni.

Amesema takwimu zinaonesha kundi la vijana linaongoza kuwa na maambukizi mapya ya Ukimwi huku wasichana wakiongoza.

Amesema kati ya waathirika watano wa Ukimwi, wanne ni wasichana kati ya miaka 15 hadi 24. Amesema mwaka 2018 wasichana  140,000 walipata maambukizi mapya ikilinganishwa na wavulana 50,000.

Akifungua kongamano hilo, naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, Antony Mavunde amesema Serikali inahitaji rasilimali za kutosha kudhibiti ugonjwa huo kupitia vyanzo vya ndani bila kutegemea wahisani.